Jaji Mkuu awaondolea mapumziko majaji, mahakimu Zanzibar

Unguja. Kutokana na mchakato wa wagombea urais na uwakilishi kutakiwa kula viapo mahakamani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla ameagiza watendaji wote wa mahakama kuwa kazini hata siku za sikukuu na mapumziko ya mwishoni mwa juma.

Hatua hiyo inalenga kuwapatia fursa wagombea wanaosaka nafasi hizo kufika mahakamani kula viapo mbele ya majaji na mahakimu.

Viapo hivyo vitaambatanishwa wakati wa kurejesha fomu za kuomba uteuzi ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, wagombea ngazi ya urais wanatakiwa kula kiapo mbele ya jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, huku wagombea nafasi ya uwakilishi wanapaswa kula kiapo mbele ya mahakimu wa mikoa.

Katika taarifa iliyotolewa na Jaji Mkuu Khamis, amesitisha mapumziko ya Sikukuu ya Maulid leo Septemba 5, na yale ya mwishoni mwa juma Jumamosi Septemba 6 na Jumapili Setemba 7 kwa majaji, mahakimu, maofisa na watendaji wengine wa mahakama ili kuhakikisha wanakuwa kazini kwa ajili ya kuwahudumia wagombea watakaofika kula viapo.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa chini ya sheria namba 2 ya mwaka 1985 na kifungu cha 27 (2), na kifungu cha tatu cha sheria namba sita ya mahakama ya mwaka 1985, siku za tarehe tano, sita na saba za Septemba mwaka huu, ambazo ni za mapumziko na wikiendi, zitakuwa siku za majaji na mahakimu, maofisa na watendaji wengine wa mahakama kuwa kazini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa ZEC, watiania wa urais na uwakilishi uchukuaji na urejeshaji wa fomu ni kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 10, 2025 saa 10:00 na siku ya uteuzi wa wagombea itafanyika Septemba 11, hivyo kuruhusu kampeni kuanza ambazo zitafanyika kwa siku 46.

Shughuli ya kuchukua fomu kwa ngazi ya urais imekamilika ambayo ilifanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 30 hadi Septemba Mosi, jumla ya watiani kutoka vyama 17 vilivyoonesha dhamira ya kushirki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu vimekabidhiwa fomu hizo.

Kwa sasa watiania hao wanazunguka mikoa yote mitano ya Zanzibar kusaka wadhamini ambako kila mkoa mgombea anatakiwa kuwa na wadhamini wasiopungua 200.

Wadhamini hao wanapaswa kuwa wanachama halali wa chama cha siasa husika. Pia, wanatakiwa kuwa wamejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura.

Wakati akiwakabidhi fomu kwa nyakati tofauti, Mweneyekiti wa ZEC, Jaji Geroge Joseph Kazi aliwaeleza wagombea miongoni mwa masharti ya ujazaji wa fomu hizo ambazo zimegawanyika katika sehemu nne, ni kula kiapo mbele ya jaji wa Mahakama Kuu.

Kwa msingi huo, iwapo ikitokea mtu akashindwa kutekeleza takwa hilo la kisheria, basi atakuwa amekosa sifa za kuwa mgombea na anaweza asiteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania urais na vyama vyao kwenye mabano ni Dk Hussein Mwinyi (CCM), Othman Masoud (ACT-Wazalendo), Mfaume Khamis Hassan (NLD) na Said Soud Said (AAFP).

Wengine ni Hamad Masoud Hamad (CUF), Hussein Juma Salum (TLP), Khamis Faki Mgau (NRA), Laila Rajab Khamis (NCCR-Mageuzi), Isha Salum Hamad (CCK), Ali Mwalim Abdalla (SAU), Juma Ali Khatib (Ada Tadea) na Mohamed Omar Shaame (UMD).

Wengine ni Shafii Hassan Salum (DP), Hamad Rashid Mohamed (ADC), Hamad Mohamed Ibrahim (UPDP), Ameir Hassan Ameir (Makini) na Neema Salim Hamad (UDP).