MASHABIKI wa Simba huko kitaani kwa sasa wameanza kuchonga. Hii ni baada ya mabosi wa klabu hiyo kufanya uamuzi unaoonekana kama unakuja kuleta mapinduzi makubwa klabuni hapo na hasa kwenye mbio za kusaka mataji katika msimu mpya wa 2025-26, huku Yanga ikitajwa.
Bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘MO’ Dewji juzi jioni aliwasapraizi mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa kutangaza kujichomoa katika Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kisha kuteua vichwa vinne matata vinavyoungana na vile vilivyokuwapo wakionekana ni sura za kazi.
MO Dewji ambaye ni Rais wa Heshima wa klabu hiyo, kabla ya uamuzi huo alikuwa akikalia kiti cha Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu kabla ya kuamua kujiengua na kukabidhi kiti hicho kwa Crescentius Magori sambamba na Mtendaji Mkuu wa zamani, Barbara Gonzalez akipewa ujumbe wa bodi hiyo.
Katika taarifa yake, MO Dewji alisema: ‘Kwa muda mrefu nimekuwa nikihudumu kama Rais wa Simba na Mwenyekiti wa Bodi, hata hivyo, kutokana na majukumu mengine na ukweli kwamba mara nyingi nipo mbali. Nimeona ni muhimu klabu yetu ipate kiongozi wa bodi ambaye yupo karibu, mwenye muda wa kutosha na anaweza kushiriki kwa ukaribu zaidi shughuli za kila siku.
“Kwa msingi huo, ninatangaza rasmi, nitaendelea kubaki kama mwekezaji na Rais wa Simba, lakini nafasi ya Mwenyekiti sasa inakabidhiwa kwa kiongozi mpya.
“Ningependa pia kutumia nafasi hii kuwashukuru kwa dhati wajumbe wote wa bodi waliotangulia kwa uongozi wao, muda na mchango mkubwa katika maendeleo ya Simba, kila mmoja wenu ameacha alama ya kipekee katika safari ya klabu yetu.
“Kwa mujibu wa katiba na kanuni za kampuni (MEMARTS) ya Simba Sports Club Company Limited, Ibara ya 41, Rais anatokana na MO Simba Company Ltd na anayo mamlaka ya kufanya uteuzi wa viongozi wa bodi, kwa mamlaka hayo, nimeamua kumteua Crescentius Magori kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba.”
Kwenye orodha mpya ya wajumbe wanane wa upande wa mwekezaji MO, amewajumuisha Magori aliyewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu na mshauri wake, sambamba na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji.
Wengine ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi na Ofisa Mtendaji mwingine wa zamani na aliyekuwa msaidizi wa Mo Dewji, Barbara Gonzalez na Profesa George Ruhago.
Wajumbe ambao wameendelea kusalia kwenye bodi hiyo ni pamoja na Rashid Shangazi, Hussein Kitta na Zuly Chandoo ambao wote watatu walikuwa sehemu ya bodi iliyopita.
Barbara, Magori, Mkwabi na Dewji wanakumbukwa na wanasimba kwa namna walivyoisumbua Yanga kwa vipindi tofauti, ikiwamo kubeba mataji manne ya mwisho mfululizo kabla ya watani wao hao kupindua meza na kufanya ‘come back’ ya aina yake misimu minne mfululizo iliyopita.
Barbara anarejea Simba baada ya kujiuzulu Januari 2023 akiwa ameiwezesha Simba kubeba mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu na kutawala soka la kimataifa hasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika akitoka kumpokea Senzo Mazingisa aliyempokea pia Magori na kubeba mataji mawili ya nyuma.
Azim Dewji anakumbukwa kwa jinsi alivyoihenyesha Yanga miaka ya 1990 na kuiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la CAF (sasa Shirikisho, baada ya kuunganishwa na lile la Washindi) mwaka 2004.
Mkwabi japo alikaa kwa muda mfupi kama Mwenyekiti wa Simba, lakini ni kati ya memba wa Friends of Simba ambao waliitingisha Yanga miaka kadhaa nyuma ikiwamo kuiburuza katika Ligi Kuu na michuano mingine waliyokutana.
Na hilo ndilo linalowafanya mashabiki wa Simba, kuamini mwisho wa ubabe wa Yanga umewadia kupitia sura hizi nne za kazi zinazoungana na wengine waliopo kuunga uongozi wa klabu hiyo.
Mabadiliko hayo, yakashtua kwa kuwatema Salim Abdallah ‘Try Again’, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, lakini akiwa pia mjumbe wa muda mrefu ndani ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kabla ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na Mohammed Nassoro.
Wajumbe hao wanane sasa wanaungana na wengine saba kuunda bodi hiyo wakitoka upande wa wanachama akiwamo mwenyekiti wa klabu hiyo Murtaza Mangungu, CPA Issa Masoud, Seleman Haroub, Asha Baraka, Dk Seif Muba na Rodney Chiduo.
Uamuzi huo wa Mo Dewji kufanya mabadiliko hayo ymepokewa vyema na Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Evodius Mtawala aliyesema MO ameunda watu wapya anaowaamini wataenda kusimamia msingi wa malengo ya mabadiliko ya Simba kiuchumi.
“Nimeona hayo mabadiliko, unajua MO amekuja Simba kama mwekezaji, maono yake alikuwa anataka kuona klabu inafanya uwekezaji ili baadaye apate faida na klabu ipate faida,” alisema Mtawala ambaye kitaaluma ni mwanasheria na kuongeza;
“Ukitazama kwa umakini utaona mabadiliko haya yanalenga kufanikisha mradi ambao unakusudiwa kufanyika baada ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.
“Angalia amewarudisha Barbara amewahi kufanya kazi Simba, Magori alikuwa mtu mkubwa serikalini, lakini amefanya kazi Simba, Mkwabi amekuwa Simba na mfanyabiashara na Azim vilevile ni mfanyabiashara mkubwa na anaijua Simba.
“Wakati nikiwa Simba bajeti yetu ilikuwa kama Sh3 bilioni tatu lakini sasa kiasi kama hicho unakizungumza kinapatikana kwenye udhamini mmoja tena wa kati.”
Pia Mtawala alisema mabadiliko hayo yanalenga Simba iweze kushindana na washindani wake wa ndani ambapo mkubwa ni Yanga, huku nje ikienda kupambana na klabu kubwa kama Al Ahly na nyingine.
“Simba inakwenda kushindana na washindani mbalimbali wa nje na wa ndani, tuangalie hapa ndani mshindani wake mkubwa ni Yanga ambaye amekuwa akipiga hatua kubwa kwa ubora, ukitazama kikosi cha Yanga utaona Simba inatakiwa kuendelea kusukwa kufikia ubora wao.
“Simba ilifanya makosa wakati ina kikosi kikubwa cha kina Chama (Clatous), Kagere (Meddie) na Bocco (John), kwa kutofanya marekebisho taratibu hadi kikaja kuanguka. Ukitazama Yanga ilijifunza na hili inaboresha kikosi chao kila hatua, Simba sasa ndio imeanzaz kujifunza, ilifanya usajili mkubwa msimu uliopita, msimu huu ikambakisha kocha yuleyule akafanya usajili wake sasa baada ya hapa bodi hii inatakiwa kuendelea kumsikiliza kocha ili akairudishe Simba imara zaidi.”
Wakati Mtawala akiyasema hayo bosi mwingine wa klabu hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe licha ya kupongeza mabadiliko hayo, lakini alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya sura za msingi kukosekana.
“Kwanza najiuliza kwanini kila wakati MO anapenda kukimbia kuongoza bodi hali ya kuwa majukumu yake hayamtaki kuwa mtu wa kuwa nchini kila wakati, unajua hata kama atakaa Ulaya bado anaweza kuongoza bodi kwa kuwa klabu ina Mtendaji Mkuu,” alisema na kuongeza; “Lingine ninaloliona walioingizwa ni watu sahihi lakini bado walihitajika baadhi ya watu kama Kaburu (Geofrey Nyange) ambaye anaweza kupambana na mtani.”
“Angalia Ulaya kwasasa klabu kubwa zinawajumuisha wachezaji wa zamani kuwa sehemu ya bodi ili kupata akili ya kiufundi, angalia Bayern Munich wanachofanya. Ni wakati wa Simba kuangalia hili ili ikitokea wanajadili ishu ya ufundi wa mpira kuwe na mtu ambaye anaaminika atatoa mchango kwa taaluma yake kuliko kuwa na watu wa biashara pekee.”