Fountain yanasa beki Mrundi | Mwanaspoti

UONGOZI wa Fountain Gate uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kati wa Namungo raia wa Burundi, Derrick Mukombozi, baada ya nyota huyo kuafikiana maslahi binafsi na mabosi wa kikosi hicho.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa kikosi hicho zimeliambia Mwanaspoti, Mukombozi amekubali maslahi binafsi na tayari amepewa mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia timu hiyo kwa msimu wa 2025-26, hivyo hadi sasa kilichobakia ni kusaini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema msimu ujao wanataka kufanya mambo makubwa zaidi tofauti na uliopita, ambapo hadi sasa kuna majina ya nyota wapya ambao watawatangaza kabla ya usajili kufungwa Septemba 7.

“Kilichotokea msimu wa 2024-25 hatutaki kukiona kikitokea tena kwa 2025-26, ni kweli tumefanya usajili mkubwa ambao tunaamini utatusaidia, tumezingatia ubora wa wachezaji katika kuwachagua na muda ukifika tutawatangaza,” alisema Wendo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mukombozi alisema hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa hadi sasa, ingawa amekiri ni kweli uwezekano wa kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-26 ni mkubwa, kutokana na ofa za timu mbalimbali zinazomuhitaji.

Nyota huyo aliitumikia Namungo kwa mkataba wa miezi sita baada ya kurejea ndani ya kikosi hicho, ikiwa ni baada ya kuondoka msimu wa 2023-24, tangu ajiunge na timu hiyo kwa mara ya kwanza Agosti 24, 2023, akitokea Nkana FC ya Zambia.

Kwa msimu wa 2023-2024, beki huyo alifunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu wa 2024-2025, alitupia moja tu katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-1 dhidi ya Mashujaa, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Aprili 20, 2025.

Beki huyo licha ya kuichezea Nkana na Namungo ya Tanzania, ila timu nyingine alizowahi kuzichezea ni Prisons Leopards ya Zambia na LLB Academic ya kwao Burundi, akitazamiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho kutokana na uzoefu wake mkubwa.