Mbeya City ile siku ndo leo

JIJI la Mbeya leo litakuwa lipo bize kutokana na uwepo wa tamasha la kijanja la klabu ya Mbeya City iliyorejea katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikitoka Ligi ya Championship.

Wanakomakumwanya leo ni siku yao na ndio maana wanashangweka kupitia Mbeya City Day kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini humo baada ya awali kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo kuchangia damu na kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa kwa zawadi mbalimbali.

Tamasha hilo litakalotumika pia kutambulisha kikosi kipya cha timu hiyo sambamba na uzi utakaotumika katika msimu wa 2025-26 litapambwa na burudani mbalimbali ikiwamo muziki kuhitimishwa na pambano la kirafiki kati ya timu hiyo na Azam FC iliyoalikwa na kutua jijini humo.

Mbeya City iliyoasisiwa Agosti 2011 na kupanda daraja msimu wa 2013-2014 na kutamba kabla ya kushuka msimu wa 2022-23, imerejea msimu huu Ligi Kuu baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi ya Championship nyuma ya vinara Mtibwa Sugar iliyoshuka pia daraja msimu wa 2023-2024.

MBE 03


Msimu uliopita timu hiyo ikiwa Ligi ya Championship, ilifanya tamasha hilo Septemba 7 mwaka jana na kucheza na Real Nakonde inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia na kuitambia kwa bao 1-0 kama ilivyofanya hivi karibuni ilipoumana nao kirafiki na kuitambia pia kwa ushindi kama huo.

Baada ya shughuli zote za wiki nzima mashabiki wa klabu hiyo na wakazi wa Mbeya kwa ujumla watajumuika pamoja kuanzia saa 4 asubuhi kwa burudani kabla ya saa 10:00 jioni kupingwa mbungi baina ya chama hilo na Azam FC ambayo hivi karibuni ilikuwa jijini Kigali, Rwanda.

Mechi hiyo ya kukata na shoka inakumbushia pambano la mwisho lililowapa Azam ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2013-14 ikiwa ni msimu wa kwanza wa Mbeya City kucheza ligi hiyo na kupoteza kwa mabao 2-1.

Licha ya kuwa ni mechi ya kirafiki ya kunogesha tamasha hilo la Mbeya City Day, lakini ni mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila moja kutaka kuonyesha heshima kwa mashabiki, Wanakomakumwanya kutotaka kuharibu sherehe na Azam kugeuzwa asusa tamashani.

MBE 01


Katika kunogesha kilele cha Mbeya City, kwa wiki nzima mashabiki na viongozi wa klabu hiyo walikuwa wakifanya shughuli za kijamii, kwa mfano Septemba 3 walitembea na kukabidhi zawadi kwa wagonjwa mbalimbali kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Kitengo cha Wazazi Meta.

Wakiongozwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Gwamaka Mwankota mashabiki hao waliweka bayana walikuwa wakirudisha fadhila kwa jamii kama sadaka kujiandaa na msimu mpya na huu ni utamaduni wao wa kila mwaka hata walipokuwa katika Ligi ya Championship.

Kati ya vifaa walivyowapa wagonjwa hospitalini hapo ikiwa ni siku chache tangu mashabiki na wapenzi wa City kuchangia damu katika Hospitali ya Igawilo Uyole ni pamoja na; pampasi, mabeseni, sabuni, mafuta na vikombe.

MBE 02


Mbeya City iliasisiwa mwaka 2011, lakini kitu cha kufurahisha ni kwamba hii ni moja ya klabu ambayo haikuwahi na kucheza Ligi ya Wilaya, Daraja la Nne, Daraja la Tatu wala La Pili kwani yenyewe iliinunua klabu ya Rhino FC ya Morogoro iliyohamishiwa Arusha.

Baada ya Rhino ikiwa Arusha kuuzwa kwa Halmashauri ya mji wa Mbeya, ndipo ikabadilishwa jina la kuwa Mbeya City ambapo ilicheza Ligi Daraja la Kwanza na msimu wa 2013 ikapanda sambamba na timu za Ashanti United ya Ilala na Rhino Rangers ya Tabora.