Maajabu ya Kundi C Kagame Cup 2025

MICHUANO ya Kombe la Kagame imeanza kwa kasi, lakini tofauti na makundi mengine, Kundi C limeonekana kuwa la kipekee baada ya timu zote nne kuanza kwa sare katika mechi za kwanza.

Katika mechi ya mapema iliyochezwa juzi Alhamisi, Kator ya Sudan Kusini ililazimishwa suluhu na Al-Ahly Wad Madani ya Sudan, kabla ya Al-Hilal Omdurman kutoka sare ya bao 1-1 mbele ya Mogadishu City ya Somalia.

Matokeo hayo yamefanya kundi hilo kuwa la pekee kati ya matatu yaliyoundwa katika mashindano haya, kwani hakuna timu iliyopata ushindi katika raundi ya kwanza.

Tofauti hiyo inajidhihirisha zaidi pale unapolinganisha na Kundi A ambapo Singida BS ilianza kwa suluhu dhidi ya Ethiopian Coffee, lakini Polisi ya Kenya iliibuka kidedea kwa kuichapa Garde-Cotes ya Djibouti mabao 4-0 zikiwa ni mechi za ufunguzi wa michuano hiyo ya 47 tangu 1967.

Kundi B pia halikukosa ladha ya ushindi, baada ya APR ya Rwanda kuifunga Bumamuru ya Burundi mabao 2-0, huku KMC ya Tanzania ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mlandege ya Zanzibar.

Kitu kingine ni kwamba hadi sasa katika michuano hiyo kabla ya mechi za jana hakuna mchezaji yeyote aliyefunga zaidi ya bao moja, kwani katika mabao 13 yote yamefungwa na mmoja mmoja tu, huku Garde Cotes ya Djibouti ikiwa ndio iliyokuwa imeruhusu mabao mengi zaidi (manne).

Mabao hayo iliruhusu katika pambano la uzinduzi wa michuano hiyo mbele ya Polisi Kenya, huku Mlandege Zanzibar ikifuata kwa kufungwa mabao matatu, ilhali KMC na Bumamuru ya Burundi kila moja ikiruhusu mabao mawili.

Wachezaji 13 waliokuwa wamefunga mabao hayo kabla ya mechi za jana ni; Eric Zakayo, David Simiyu, Baraka Badi na Edward Omondi (wote wa Polisi Kenya), Djibril Aouttara na William Togui wa APR,  Juma Mwita Sagwe, Rashid Chambo na Abdallah Lanso wote wa KMC. Pia kuna Abed Ama na Aimar Hafidh wote wa Mlandege, Emmanuel Flomo wa Al Hilal na Mark Khadohi wa Al Ahly Madani, akiwa ndiye pekee aliyefunga kwa mkwaju wa penalti kabla ya jana.