UONGOZI wa Coastal Union uko katika mazungumzo ya kumsajili aliyekuwa beki wa Pamba Jiji, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ baada ya nyota huyo kumaliza mkataba, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine mpya wa kukichezea tena kikosi hicho.
Nyota huyo wa zamani wa Mashujaa ameshindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya na Pamba ambapo kwa sasa inadaiwa ‘Wagosi wa Kaya’ wanaamini ni mbadala sahihi wa Miraji Abdallah ‘Zambo Jr’ aliyejiunga na Dodoma Jiji.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza Oviedo yupo hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho cha Coastal Union kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, huku kilichobaki ni kusaini tu kukitumikia.
“Baada ya kuondoka ‘Zambo Jr’ tunataka kuongeza mchezaji mwingine mzoefu anayeweza kuziba nafasi yake ipasavyo. Oviedo ni chaguo sahihi kwetu na hata benchi letu la ufundi limemridhia ili kuongeza nguvu msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Kikosi hicho hadi sasa kimekamilisha baadhi ya wachezaji wapya ambao hata hivyo hakijawatangaza wakiwemo Ally Ramadhan Kagawa, Jonathan Ulaya (Geita Gold), Jofrey Manyasi, Cleophace Mkandala (Kagera Sugar) na Jonas Manyama wa Chipukizi.
Wengine ni Mahmoud Haji Mkonga ‘Aguero’ (Mlandege), Wilbol Maseke (KMC), William Andrew (Stand United), Adam Salamba (Branes SC), Lassa Kiala (KenGold) na Robert Pius Salula ‘Morrison’ aliyetokea Mwembe Makumbi City ya Zanzibar.
Nyota mwingine ni aliyekuwa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar na Mashujaa, Athumani Masumbuko ‘Makambo Jr’ aliyerejea nchini baada kuondoka na kwenda kuzichezea 1. FCA Darmstadt na SC Viktoria 06 Griesheim za Ujerumani.