Bado Watatu – 20 | Mwanaspoti

ALINIPENDA sana na mimi nilimpenda. Alikuwa mwaminifu kwangu na mimi nilikuwa mwaminifu kwake. Alikuwa akisafiri kwa wiki mbili au tatu na kuniacha. Sikuwa na ushawishi wowote wa mwanaume na niliamini huko alikokwenda na yeye hakushawishika na wasichana.
Miongoni mwa marafiki zake Sufiani ambao alikuwa akifika nao pale nyumbani alikuwa jamaa mmoja aliyekuwa akiitwa Shefa. Shefa alikuwa ni dereva na aliwahi kufanya kazi katika kampuni moja na Sufiani, lakini baadaye alipata pesa akajenga nyumba yake maeneo ya Mikanjuni kisha akanunua lori lake mwenyewe. Akaacha kazi ya kuajiriwa, akawa anaendesha lori lake.
Sufiani anaporudi Tanga kutoka safari zake ni lazima arudi nyumbani akiwa na Shefa. Hapo huwawekea chakula au vinywaji na tunakula kwa pamoja na kuzungumza hili na lile.
Mara nyingi mume wangu alikuwa akimhoji Shefa kuhusu maendeleo yake. Nilihisi kwamba alipenda kuwa pamoja na Shefa mara kwa mara ili na yeye aweze kuzijua mbinu alizotumia mwenzake mpaka akaweza kujenga nyumba na kununua lori lake mwenyewe akiwa ameajiriwa kama dereva.
Lakini kwa madereva wa malori wanaokwenda nje ya nchi hilo linawezekana kama dereva mwenyewe ataweka nia na dhamira. Posho wanayopewa wanapokwenda nje ni kubwa na hukaa huko wakati mwingine kwa wiki mbili au tatu.
Lori linaporudi tupu mara nyingi hutafuta mzigo wa kuuleta nchini ambao tajiri anakuwa hajui. Huo anaujua dereva na mataniboi wake.
Kwa hiyo, kwa dereva aliyeweka nia ya kujenga angeweza kufanya hivyo kwa kuweka pesa zake kidogo kidogo.
Lakini Shefa hakuishia kujenga tu, baadaye aliweza kununua lori lake mwenyewe. Alikuwa akimwambia mume wangu kuwa alijinyima na kuacha starehe ndipo aliweza kununua lori hilo. Lakini pamoja na ukweli huo tulishuku kuwa kulikuwa na kitu kingine kilichochangia apate lori hilo.
Kulikuwa na kipindi fulani, Sufiani alipata mzigo wa kupeleka Burundi. Alikaa huko karibu wiki tatu. Tulikuwa tukiwasiliana kwenye simu, akaniambia kwamba alichelewa mpakani wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kwa sababu kulikuwa na foleni ndefu za magari.
Aliporudi ilikuwa saa tano mchana. Akanipigia simu akiwa Dar na kuniambia kuwa mpaka saa kumi na mbili jioni atakuwa ameingia Tanga.
Saa kumi na mbili jioni sikumuona. Nikasubiri hadi saa moja nikampigia simu.
“Uko wapi?” nikamuuliza.
“Niko hapa Saba Saba, niko na Shefa,” akaniambia.
Alipotaja Saba Saba nikajua kuwa walikuwa katika eneo la Uwanja wa Saba Saba uliopo Gofu, ambapo palikuwa na baa ambayo walipendelea kwenda kunywa bia.
“Umeingia saa ngapi?” nikamuuliza.
“Saa kumi na mbili.”
“Sasa kwanini unafikia baa badala ya kufika kwanza nyumbani kwako?”
“Nilipokuwa nakuja Shefa alinipigia simu akaniambia ananisubiri hapa. Tulikuwa na mpango fulani wa pesa, ndiyo tunauzungumzia.”
Nikajua alikuwa akinidanganya. Walikuwa wanakunywa na hawakuwa na mpango wowote wa pesa.
Mara kadhaa nilikuwa nikimkataza Sufiani apunguze ulevi lakini alikuwa hanisikii. Kisingizio chake kikubwa ni kuwa ananunuliwa na Shefa. Lakini huo ulikuwa ni uongo wake. Jinsi alivyokuwa akijipendekeza kwa Shefa, yeye ndiye aliyekuwa akimnunulia pombe.
“Sasa utakuja saa ngapi huku?” nikamuuliza.
“Baada ya nusu saa tu nitakuwa nimeshafika.”
Ilikuwa ni kweli, baada ya nusu saa Sufiani akaja nyumbani lakini hakuwa peke yake. Alikuwa na rafiki yake Shefa.
Wote wawili walikuwa wamelewa. Shefa ndiye aliyelewa sana.
“Shem, wewe umeshafanikiwa, mwenzako bado anajikongoja. Kila siku namkataza kulewa. Anapoteza pesa nyingi ambazo tunazihitaji kutuletea maendeleo,” nikamwambia Shefa kidogo nikionesha hasira.
Nilijua maneno yale yatawauma wote wawili lakini ilibidi niwaambie ili wajue kuwa sipendi kumuona mume wangu akinywa pombe.
“Shem usiseme hivyo. Mume wako hakutumia hata senti tano yake. Nimemnunulia mimi leo,” Shefa akajihami haraka huku akiketi.
“Bora umwambie wewe. Mimi nikimwambia haniamini. Kwanza pombe yenyewe nimekunywa chupa moja. Tangu aanze kunikataza nimeacha kunywa sana,” Sufiani akaniambia.
“Mwongo wewe. Hujakunywa chupa moja. Tangu saa kumi na mbili uliyofika umekunywa chupa moja tu?”
“Tulikuwa na mazungumzo mke wangu. Tulikuwa na tajiri ambaye anataka kutupa kazi ambayo itatupatia pesa nyingi.”
“Hakuna lolote. Mbona nilipokupigia hukuniambia kama kuna tajiri mnaongea naye? Mimi najua mlikuwa mnakunywa tu, lakini unashindana na Shefa. Mwenzako ameshajiweka vizuri. Shauri yako!”
Shefa alitoa kicheko cha uongo huku maneno yangu yakiwa yamemuumiza.
“Nimejiweka vizuri wapi shem wangu. Mimi na Sufiani tuko sawa tu,” akaniambia.
“Hamko sawa. Wewe una nyumba yako, mwenzako bado anaishi kwenye nyumba ya kupanga na hana hata matarajio ya kujenga nyumba yake…”
“Sasa shem wangu, kile kibanda ndiyo utaita nyumba? Hujaziona nyumba za watu. Hujakwenda Raskazoni ukaona majumba?”
“Hicho kibanda unachosema sisi hatuna. Angalau wewe una kibanda, sisi tuna nini? Tutaishia kupanga katika nyumba za watu hadi lini?”
“Tuombe Mungu. Mtapata tu.”
“Sasa kama mtindo ndiyo huo, hatutapata.”
“Amini Mungu, mume wako hajanunua pombe. Nimemnunulia mimi na ni chupa moja tu aliyokunywa. Asingeweza kukaa pale wakati wenzake tunakunywa.”
“Yamekwisha, lakini najua ujumbe ameupata.”
“Kama yamekwisha, umepika nini?”
“Sijawawekea chakula. Uliponiambia mko Saba Saba nikajua mtakula huko huko na pia hukuniambia kama utakuja kula.”
Sufiani ni mkimya sana, akanyamaza. Lakini kama ingekuwa mtu mwingine angejitia kugomba.
“Ngoja basi niwatayarishie chipsi,” nikawaambia.
“Chipsi na nini?” Sufiani akaniuliza.
“Kitu cha haraka ni chipsi na mayai.”
“Tutayarishie basi,” Sufiani akaniambia kisha akamtazama Shefa.
“Shefa, utakula chipsi?”
“Atutayarishie tu.”
Baada ya kunikubalia kwamba watakula chipsi niliingia jikoni. Nilimenya viazi na kuvikatakata vipande vipande. Baada ya dakika chache tu nikawa ninakaanga chipsi.
Sufiani na Shefa walikuwa wakiendelea kuzungumza sebuleni. Baada ya chipsi kuwa tayari, nilivunja mayai nikatayarisha sahani tatu za chipsi. Kila sahani moja niliikaangia mayai mawili.
Nilipomaliza niliwawekea tomato, pilipili kidogo na ukwaju. Nikawapelekea.
Nikawawekea na juisi ambayo niliitoa kwenye friji.
Zilikuwa sahani tatu, moja ilikuwa yangu mwenyewe. Nilikuwa nimeshakula lakini zile chipsi na mayai zilinitia hamu ya kula tena.
Wakati wanakula niliwawekea movie ya kibabe kutoka Marekani. Wote wawili walikuwa wabovu sana wa sinema za kimapigano.
Tukaendelea kula huku tukitazama sinema. Chipsi zilikwisha, sinema ilikuwa bado ikiendelea.
Tuliitazama mpaka mwisho wake. Shefa akaniaga. Mume wangu akamsindikiza.
Baada ya muda kidogo mume wangu alirudi na hapo ndipo tulipoulizana habari za safari.
“Mwenzangu, siku hizi ukirudi hufikii nyumbani, unaishia mabaa,” nikamwambia Sufiani.
“Si nimekwambia Shefa alinipigia simu tangu nikiwa njiani akaniambia ananisubiri pale Saba Saba. Kulikuwa na mtu tuna mipango naye ya kazi.”
“Hiyo mipango ni mipango ipi?”
“Ni mipango ya kazi. Huyo mtu ana mzigo wake anataka upelekwe Nairobi, lakini tumepanga akienda ofisini aseme kuwa mzigo huo unashushwa Mombasa halafu sisi tunaupeleka Nairobi.”
“Sasa ni kwanini mnataka adanganye?”
“Pale ofisini atalipa pesa ya kushusha mzigo Mombasa. Ile pesa ya kuupeleka Nairobi atatulipa sisi, yaani tunamtoza nusu ya pesa ambayo angetozwa na tajiri.”
“Mmeshakubaliana?”
“Tumeshakubaliana. Lakini huo mzigo utapatikana wiki ijayo. Unajua nimegundua Shefa alikuwa na njia nyingi za kumpatia pesa hadi akaweza kununua lori lake. Hizi dili ndiyo alikuwa anazicheza sana.”
“Basi na wewe ukazane tujenge nyumba.”
“Tutajenga tu mke wangu wala usijali.”
Baada ya mazungumzo marefu tukalala.
Asubuhi kulipokucha Sufiani alitoka. Kwa kawaida kama Sufiani hakwenda safari huwa nashinda nyumbani. Siendi kazini kwangu kwa vile kuna wasichana wanaonifanyia kazi.
Kwa hiyo baada ya Sufiani kutoka nilishughulika na mapishi ya mchana.
Wakati niko jikoni mke wa Shefa akanipigia simu. Tulikuwa tunafahamiana ingawa hatukuwa na uhusiano wa karibu sana.
Baada ya kusalimiana naye aliniuliza:
“Eti, mume wangu alikuwa nyumbani kwako jana usiku?”
“Ndiyo, alikuwa kwangu. Kwani vipi?”
“Jana alirudi usiku mwingi mpaka nikapata wasiwasi. Nilipomuuliza unatoka wapi akaniambia alikuwa nyumbani kwa Sufiani na alikula huko huko.”
“Ni kweli. Alikuja na mwenzake nikawaandalia chakula. Tukazungumza sana…”
“Basi sikumuamini. Nilivyoona amelewa nikajua anatoka kwenye michepuko yake. Si unajua hawa madereva wa malori hawaaminiki.”
“Ni kweli, lakini kwa jana alikuwa kwangu. Mimi pia nawadhibiti sana.”