Kipa aliyevunjika taya aanza mazoezi mepesi

KIPA wa Tabora United, Fikirini Bakari amerejea uwanjani baada ya kuwa nje akijiuguza kutokana na kudaiwa kuvunjika taya

wakati akikiwasha katika mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga iliyowafunga mabao 4-0 wiki iliyopita katika Uwanja wa  Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Fikirini alisema daktari alimwambia afanye mazoezi mepesi ya kukimbia na kuepuka kukongana na watu, na baada ya wiki mbili anapaswa kurejea hospotali kujua maendeleo ya afya yake.

“Wakati naruka kuokoa mpira niligongana na mtu nikavunjika taya ambapo hospitali waliniwekea nyaya za kukaza taya ili zirudi katika hali ya kawaida, baada ya wiki mbili nitaambiwa maendeleo yangu na kipi nikifanye,” alisema Bakari na kuongeza:

“Kwa upande wa vyakula kwa sasa naruhusiwa kutumia mtori na juisi hadi nitakapokaa sawa. Maumivu yanapungua tofauti na nilivyokuwa najisikia mwanzo.”

Kipa huyo aliyemaliza na bila kuruhusu bao katika mechi moja alipokuwa akuicheza kwa mkopo Fountain Gate akitokea Singida Black Stars kisha akapelekwa tena kwa mkopo Tabora United kupitia dirisha dogo, alisema anaamini atapona kabisa na kurejea katika majukumu yake.

“Ni changamoto za kazi. Jambo la msingi nazingatia maagizo ya daktari ili niweze kupona kwa uharaka na kurejea katika kazi zangu,” alisema.