Raizin ataka 10 zaidi Bara

MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema malengo aliyojiwekea msimu huu katika kikosi hicho ni kufunga zaidi ya mabao 10, huku akidai endapo atatimiza hayo itakuwa ni njia nzuri kwake kuwa na mwendelezo mzuri.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa sehemu ya kuirudisha Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara alimaliza Championship akiwa kinara wa upachikaji wa mabao akiingia kambani mara 18 sawa na Andrew Simchimba aliyetimkia Singida Black Stars akitokea Geita Gold.

Mchezaji huyo aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea Dodoma Jiji ameliambia Mwanaspoti kuwa anatambua ameingia katika ligi bora yenye ushindani, hivyo malengo yake ni kufunga mabao 10 na kuisaidia Mtibwa Sugar kuwa na msimu bora baada ya kurudi Ligi Kuu Bara ikiahidi kuandika rekodi ya kumaliza nafasi tano za juu.

“Natamani kufunga zaidi ya mabao 10. Natambua nimetoka kuibuka kinara Championship, haikuwa rahisi kutokana na changamoto ya ugumu wa ligi hiyo. Sasa tumerudi ligi namba nne kwa ubora Afrika huku kuna ushindani mkubwa zaidi, lakini nimejiandaa na maandalizi yanakwenda vizuri. Natamani kufikia malengo,” alisema.

“Siyo rahisi, lakini naamini ili malengo yatimie ni kuwekeza juhudi kwenye upambanaji na ili kuonyesha kuwa sikubahatisha kufanya vizuri Championship natakiwa kuendeleza juhudi zangu huku mabao 10 siyo haba, huu ni mpango wa mwanzo tu nikipata nafasi zaidi nitafunga.”

Raizin aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwemo Gwambina na Coastal Union, anawaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwaunga mkono kwani Championship walikotoka walipata nguvu kupitia wao, hivyo wanahitaji sapoti zaidi kutokana na ushindani mkubwa uliopo.