CCM na vita halali kusaka dola, Chadema ikisubiria Oktoba 29

Dar es Salaam. Chadema kususia Uchaguzi Mkuu 2025 na ajenda yao ya No reforms no election, vyama vingine vyote kushiriki na mifumo ya nchi kuielekea Oktoba 29, 2025 kuhakikisha wananchi wanapiga kura, ni taswira kuwa mwaka huu ni zaidi ya uchaguzi.

Nani yupo sahihi na yupi mtazamo na msimamo wake vinavuta zaidi umma? Swali hilo ndilo linalopita katikati ya tafsiri kuwa Uchaguzi Mkuu 2025 si wa mashindano ya msuli wa majukwaani na kwenye sanduku la kura, bali ni vita ya maonyesho na matokeo ili kupigania uhalali.

Battle of legitimacy au kwa Kiswahili, vita ya uhalali ni mapambano ya kupata au kuhodhi uungwaji mkono. Ni msako wa kukubalika kwa mamlaka, dola, taratibu za kimfumo na michakato ya kidola mbele ya umma.

Uchaguzi ni utaratibu wa kimfumo kwa sababu ni maelekezo ya Katiba ya nchi, vilevile ni mchakato wa kidola, maana mihimili miwili ya dola – Serikali na Bunge – inapatikana kupitia uchaguzi. Mhimili mmoja, Mahakama, upatikanaji wake wake unategemea Serikali.

Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho kinaongoza dola na mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan, kwa hali halisi hawashindani na upinzani kuelekea sanduku la kura tu, bali vita ya sasa ni uhalali wa uchaguzi, kisha uhalali wa kuchaguliwa.

Chadema, chama kikuu cha upinzani Tanzania, kupitia ajenda yake ya No reforms no election, yaani bila mabadiliko ya Katiba kwenye maeneo yahusuyo uchaguzi na sheria ya uchaguzi katika vifungu mahususi, hakuna uchaguzi. Bila shaka, msimamo huo unatokana na imani yao kwamba wana nguvu ya umma.

Kwa Chadema kususia uchaguzi, maombi na matumaini yao ni kuona wananchi kwa wingi wao waone Uchaguzi Mkuu 2025 hauna maana yoyote, hivyo wasusie mikutano ya kampeni, vilevile siku ya kupiga kura, vituo viwe vyeupe.

Ususiaji wa mikutano ya kampeni, vituo kuwa vyeupe siku ya kupiga kura, kisha hesabu ya waliojitokeza kupiga kura kuwa chini ya asilimia 50, itawafanya Chadema watunishe vifua kwamba wameweza kuufanya umma uukatae uchaguzi.

Kwa vipimo, idadi ya wanaojitokeza kupiga kura inapokuwa chini ya asilimia 50 ya namba ya wapigakura walioorodheshwa kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura, uchaguzi huo huhesabiwa umefeli. Kwa mantiki hiyo, Chadema wanaangazia matokeo ya kufeli kwa uchaguzi, CCM wanasaka ufaulu.

Kufana kwa Uchaguzi Mkuu 2025 litakuwa pigo kwa Chadema. Mikutano ya kampeni kuvutia watu wengi na idadi ya wapigakura kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, itakuwa shambulio kali kwa Chadema na itakiweka chama hicho kwenye wakati mgumu wa kusimamisha ajenda zake.

Kufeli kwa Uchaguzi Mkuu 2025, kutajenga afya, ari na kujiamini kwa Chadema kuendelea kuwa mhusika muhimu wa siasa za nchi. Kinyume chake, chama hicho kitatakiwa kujiuliza kuhusu nafasi yake kwa umma, endapo msimamo wake wa kususia uchaguzi hautakuwa na athari yoyote kwa umma.

Uhalali unaweza kupatikana kwa mahaba, imani, hofu, sheria, vilevile propaganda. Umma unapompenda kiongozi, bila shaka watakubali mamlaka yake. Kuna imani, ukiaminika utafuatwa, hivyo uongozi wako utaaminika.

Upo uhalali unaotokana na hofu. Mnajua kuwa mkipinga mamlaka kuna cha mtema kuni mtakutana nacho. Hofu hiyo inaweza kuwa ni dhidi ya mamlaka husika au yajayo baada ya mabadiliko. Mwisho, umma unaamua kutulia na kutii mamlaka.

Mamlaka ambazo zinapatikana kwa kufuata sheria halali na taratibu zilizowekwa, moja kwa moja hupata uhalali, japo ipo nafasi ya propaganda. Mamlaka ikishikiliwa na watu mahiri, wenye utaalamu wa propaganda, huweza kushawishi uhalali hata mahali ambapo awali hawakuwa wakikubalika.

Wataalamu wa propaganda wakiwa nje ya mamlaka, wanaweza kutengeneza ushawishi mkubwa kwa umma, hivyo kuifanya mamlaka ikose uhalali. Vita ya uhalali inapopiganwa, pamoja na kutumia kila nyenzo, kwa sehemu kubwa propaganda hutakiwa kuchezwa inavyotakiwa.

Ilihitaji maarifa makubwa ya propaganda ili kuituliza Iran baada ya mapinduzi yaliyomwondoa madarakani aliyekuwa mtawala wa taifa hilo la Kiajemi, Mohammad Pahlavi na kuhitimisha zama za utawala wa Shah. Kazi kubwa ilifanywa na mwanamapinduzi, vilevile mwanafalsafa, Ruhollah Khomeini.

Chini ya mwongozo wa Khomeini, ambaye ni Ayatollah (kiongozi mkuu) wa kwanza Iran, uwekezaji mkubwa wa propaganda ulifanyika. Ni propaganda hizo zilizosababisha Khomeini kuwa kiongozi pendwa na mbeba maono na matumaini ya Waajemi. Dola ya Kiislamu ya Iran ikapata uhalali mkubwa mbele ya umma.

Machapisho mbalimbali yaliandikwa kutoka Iran, yakatumika kufundisha watoto wa Kiajemi, yakajenga maambukizi kwa vizazi hadi vizazi. Machapisho hayo yalitafsiriwa kwa lugha mbalimbali, kueleza misimamo yao, wanachopigania na adui wao wa kimsingi. Hiyo ni sababu ya Iran kuwa taifa imara na linaloungwa mkono sehemu kubwa duniani. Ni matokeo ya kazi ya kipropaganda.

Ibrahim Traore, aliichukua nchi ya Burkina Faso kijeshi. Hulka yake ya kufanya siasa za umaarufu ilimfanya akubalike haraka na kuwafanya Wabukinabe wamwone ndiye mbeba maono wao, mtetezi na aliyeshikilia matumaini ya vizazi vijavyo vya nchi hiyo. Dunia nzima Traore anaimbwa. Ni nguvu ya propaganda.

Iran ya Khomeini kisha Ayatollah Ali Khamenei, aliye madarakani sasa, hadi Traore wa Burkina Faso, ni mifano kuonyesha kwamba propaganda ni karata muhimu katika kujenga kukubalika. Umma hufuata mkumbo wa kupenda au kuchukia. Kujenga uhalali ni maarifa, ni sanaa, lakini pia sayansi inahitajika.

Karata ya propaganda ni mchezo wa kujenga au kubatilisha uhalali kwa watu. Uchaguzi Mkuu 2025, unahitaji zaidi sanaa na sayansi za kipropaganda katika msako wa uhalali.

Katika msako wa uhalali wa uchaguzi, haitakiwi mikutano ya CCM peke yake ndiyo ionekana inashona mafuriko ya watu. Vyama vingine, vinatakiwa kupata watu ili angalau kuthibitisha kuwa mwitikio wa uchaguzi upo, tena mkubwa.

Idadi ya watu kwenye mikutano ya kampeni haina maana ya kukubalika kwa vyama na wagombea peke yake, bali pia huashiria utayari wa watu kushiriki uchaguzi.

Umma unahudhuria mikutano ili kusikiliza sera na ahadi za vyama na wagombea. Mikutano ya uzinduzi wa kampeni za vyama vya upinzani, Chaumma, viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam; CUF, Furahisha, Kirumba, Mwanza; pamoja na vingine ambavyo tayari vipo ulingoni haijatoa nuru.

Mikutano ya CCM, kupitia mgombea wake wa urais, Samia na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, ndiyo ambayo inatoa nuru kwamba kuna kundi kubwa la Watanzania, lipo kwenye utayari wa kushiriki uchaguzi.

Tayari siku saba zimekamilika tangu Tume Huru ya taifa ya Uchaguzi (INEC) ifungue pazia Agosti 28, 2025. Siku zinakwenda, itafika tarehe ya uchaguzi (Oktoba 29). Kitu ambacho kinatakiwa kupata zingatio kubwa ni kwamba, kimazingira na hali halisi ilivyo, Uchaguzi Mkuu 2025 ni mapambano ya msako wa uhalali.

Chadema na wanaokiunga mkono chama hicho wanataka kuthibitisha kukubalila kwa ajenda yao No reforms, No election, kwenye uso wa jamii.

CCM na vyama vingine 17 wanatakiwa kuthibitisha kwamba, Watanzania wapo tayari kwa uchaguzi, vilevile mwitikio wa upigaji kura, uonyeshe kuwa Chadema si kikwazo cha uchaguzi. Kwamba No reforms, No election ni ajenda ya wachache.