KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema licha ya ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya Kenya Police katika mashindano ya Kombe la Cecafa Kagame, bado kuna maeneo muhimu ambayo timu inahitaji kuboresha ili kuwa bora zaidi.
Gamondi ambaye anatumia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao, alisema mechi hiyo iliwapa changamoto juzi na kuwalazimu kubadili mbinu tatu tofauti za uchezaji.
“Ni wazi kuwa tunaendelea kuwa bora, lakini bado kuna maeneo ya kuboresha. Tunahitaji kuendelea kubadilika na kuendana na jinsi mchezo unavyotegemea kila hatua,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.
Alieleza kuwa kila mchezaji anatakiwa kuelewa jukumu lake vizuri, kwani mara nyingine wa umakini usipozingatiwa unaweza kuathiri matokeo.
“Tunahitaji kuhakikisha kila mchezaji anajua nafasi yake na jinsi ya kushirikiana na wenzake. Hii ndiyo njia ya kuimarisha mashambulizi na ulinzi wetu,” alisema Gamondi ambaye katika mechi hiyo alimtumia kiungo wake, Morice Chuku kama beki wa kati.
Katika mechi mbili zilizopita za mashindano ya Kagame, kocha huyo alikosa huduma za wachezaji muhimu akiwemo Khalid Aucho na Marouf Tchakei ambao wapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
Wachezaji hao kwa mujibu wake wana mchango mkubwa katika kuongeza nguvu na ubora wa kikosi hicho na kurejea kwao kutakuwa na maana kubwa katika malengo ya timu.
Kocha huyo alikiri kwamba kuna wakati wanashindwa kudhibiti mchezo kutokana na wachezaji wake kutozoeana vya kutosha, jambo linalosababisha makosa ya mara kwa mara uwanjani.