Mwalimu aahidi SGR Kanda ya Kaskazini kuinua biashara ndogo, utalii

Moshi. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi pindi akichaguliwa kuongoza nchi, atahakikisha ujenzi wa mtandao wa reli ya kisasa (SGR) katika Kanda ya Kaskazini, ili kuchochea maendeleo ya biashara ndogo ndogo na kukuza sekta ya utalii katika eneo hilo.

Akizungumza jana, Ijumaa, Septemba 5, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Manyema, Manispaa ya Moshi, Mwalimu alisema biashara ndogo ndogo zimekuwa zikikumbwa na changamoto kubwa ikiwemo kodi na tozo zisizo rafiki, pamoja na ukosefu wa sera madhubuti za kuwawezesha wajasiriamali wadogo.

 “Tunataka kufungua mjadala na wataalamu na wafanyabiashara ili tupunguze kodi na tozo zisizo za lazima. Biashara ndogo kama wauza matunda, mamalishe na saluni wanakosa msaada wa kisheria na sera. Hii inasababisha biashara nyingi kufa badala ya kuimarika,” amesema.

Mwalimu amesema SGR ikishajengwa kwenye ukanda huo, itarahisisha usafiri wa bidhaa na watalii, hivyo kuongeza mapato kwa wafanyabiashara wadogo na kukuza uchumi wa eneo hilo.

 “Sekta ya utalii ndiyo uti wa mgongo wa kanda hii baada ya kilimo. Ndani ya miaka mitano, SGR itafika Arusha na Kilimanjaro, tukirahisisha usafiri na kuongeza idadi ya watalii,” alisema.

Baadhi ya wananchi wakifuatilia mkutano wa kampeni wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) uliofanyika jana Ijumaa, Septemba 5, 2025, katika Uwanja wa Manyema, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.



Aidha, mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia Chaumma, Patrick Assenga alisema vipaumbele vyake ni pamoja na kurejesha hadhi ya mji wa Moshi kuwa miongoni mwa miji safi zaidi barani Afrika.

Vipaumbele vingine ni kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi na miundombinu ya mji, kuondoa kodi na tozo zisizo na tija, pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wamachinga, ili waweze kustawi bila kubughudhiwa.

“Tunatakiwa tupate mtu atakayepigania bungeni masilahi ya Moshi. Kazi hii nitumeni mimi; rekodi zangu zinafahamika, napigania wananchi, na sio chawa. Watanzania wamechoka kusimuliwa stori, nchi hii ni tajiri, si maskini,” alisema Assenga.

Akizungumzia sera za mgombea urais wa Chaumma, Sara Mosha, mkazi wa Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, amesema ikiwa kweli mradi wa SGR utatekelezwa, unaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa biashara ndogo ndogo na sekta ya utalii katika kanda hiyo.

Alieleza kuwa changamoto kama kodi nyingi, tozo zisizo na msingi, pamoja na ukosefu wa sera za kuwalinda wafanyabiashara wadogo, vimekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa biashara ndogo mjini Moshi.

“Mfanyabiashara mdogo hana nafasi ya kushika soko kwa sababu kila hatua anakumbana na vikwazo. SGR itarahisisha usafirishaji wa bidhaa na watalii, na hivyo kuongeza mapato na kukuza uchumi wa kanda yetu,” alisema Mosha, ambaye alikuwa miongoni mwa walioudhuria mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Moshi.