Ayelifunga hat-trick aichimba mkwara Polisi Kenya

MSHAMBULIAJI wa Ethiopian Coffee, Amanuel Admassu ambaye alipachika mabao matatu ‘hat-trick’ ya kwanza kwenye mashindano ya Kombe la Cecafa Kagame, ameichimba mkwara Kenya Police ambayo watakutana nayo katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi.

Admassu alipachika mabao hayo, akisaidia Ethiopian Coffee kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Garde Cotes ya Burundi katika mechi ya Kundi A iliyopigwa Ijumaa kwenye uwanja wa KMC.

“Nimefurahi sana kwa mchezo mzuri tuliouonyesha na mabao mengi tuliofungwa. Hii inatupa motisha kuelekea mechezo wetu wa mwisho wa kundi dhidi ya Kenya Police,” alisema mshambuliaji huyo.

Admassu alifunga hat-trick hiyo katika dakika ya 37, 45+2 na 57, mabao mengine ya Ethiopian Coffee katika mechi hiyo yalifungwa na Abubakar Adamu na Zelalem Abate ambaye alifunga mawili.

Kwa upande wake. kocha wa Ethiopian Coffee, Abiy Kassahun alieleza umuhimu wa ushindi huo.

“Tunapaswa kuendelea kuwa makini, lakini timu ni wazi kuwa timu imenifurahisha kwa kiwango cha mchezo leo. Mabao haya yatatupa nguvu ya kuendelea na mchezo wetu ujao,” alisema.

Kwa matokeo hayo, Ethiopian Coffee ndio kinara wa kundi A ikiwa na pointi nne sawa na Singida BS, Polisi inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu huku Garde Cotes ikiburuza mkia.