JAMIIFORUMS YAFUNGIWA KWA SIKU TISINI

 ::::::

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda wa siku 90 leseni ya huduma za maudhui mtandaoni iliyokuwa inamilikiwa na kampuni ya Vapper Tech Limited, wamiliki wa jukwaa maarufu la JamiiForums, baada ya tuhuma za kuchapisha maudhui yanayodaiwa kupotosha na kudhalilisha viongozi wa Serikali. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 6, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, mamlaka hiyo imeeleza kuwa Septemba 4, JamiiForums ilichapisha taarifa mtandaoni ambazo kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025, kwa madai ya kushusha heshima ya Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Aidha, TCRA imesema maudhui hayo hayakuvunja tu kanuni, bali pia yanakiuka mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania kwa kuathiri mshikamano wa kitaifa, hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikikano wa kijamii.

 “Kutokana na mamlaka tuliyopewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, TCRA imesitisha kwa muda wa siku tisini (90) kuanzia leo, Leseni ya Huduma za Maudhui Mtandaoni iliyotolewa kwa Vapper Tech Limited (JamiiForums),” inasema sehemu ya taarifa hiyo