Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Jo-seph Warioba amesema licha ya ahadi za kuvutia kuhusu uanzishwaji wa mchakato wa Katiba mpya, nyuma ya kauli hizo kuna kikwazo cha utashi wa kisiasa kinachodhoofisha upatikanaji wake.
Amesema kutokana na kikwazo hicho mara nyingi tume na taasisi zinazoundwa kuhusiana na suala hilo, huegemea zaidi katika masilahi binafsi ya walioteuliwa na waliowateua badala ya kuakisi matakwa ya wananchi, hali inayochochea mkwamo wa mara kwa mara.
Jaji Warioba amesema hayo akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu: “Taasisi za Utunzi wa Katiba: Asili, Uundwaji, Mamlaka na Majukumu Yao” kilichoandikwa na Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Sa-laam (UDSM), Dk Idd Mandi.
Amesema changamoto kubwa katika safari ya Katiba mpya ni ukosefu wa dhamira ya dhati kutoka kwa wanasiasa.
“Kwa muda mrefu tangu mwaka 1992 tume zimekuwa zikiundwa kwa msuku-mo wa nje na si kwa utashi wa kisiasa. Ndiyo maana mapendekezo yake yamekuwa yakipuuzwa, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mapendekezo ya Tume ya (Francis) Nyalali,” amesema Warioba.
Amesema tume zilizoundwa kwa misingi ya utashi wa kisiasa, kama ile ya Rashid Kawawa na Thabit Kombo wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza, zilifanikiwa kwa sababu zilitegemea nia ya kweli ya viongozi waliokuwa madarakani.
Jaji Warioba akizungumzia kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini, amesema wagombea urais na wagombea wenza wamekuwa wakiahidi kufufua mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, kwa nia ya kupata tu kura za wananchi, lakini si kwa uhalisia wa ku-pata Katiba.
Amekosoa wanasiasa wanaotumia ma-jukwaa ya kampeni kuahidi kufufua mchakato wa Katiba mpya kwa nia ya kupata kura badala ya dhamira ya dhati.
“Baadhi wanadai ndani ya siku 100 za urais wataanzisha maridhiano kwa ajili ya Katiba mpya. Ni kauli zinazotia moyo, lakini kimsingi haziwezekani bila maan-dalizi na maridhiano ya kweli. Tusisubiri uchaguzi, tuanze sasa,” amesema.
Amesema wananchi wamekuwa wakipuuzwa kwa muda mrefu, jambo linalohatarisha mustakabali wa Taifa.
“Kuanzia mwaka 1992 mawazo ya wananchi yamepuuzwa. Tukifika mwaka 2030 bila Katiba mpya ya wananchi, nchi inaweza kutetereka amani yake,” ame-onya.
Jaji Warioba, ambaye ni mwanasheria mkongwe nchini, aligusia namna Rais Samia Suluhu Hassan alivyoanzisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya kwa kuunda tume, lakini baadaye kukatokea mkwamo baada ya waziri (ha-kumtaja jina) kujitokeza na kusema kunahitajika miaka mitatu, ili wananchi wapewe elimu kuhusu Katiba kwanza.
“Mimi naamini baada ya uchaguzi, ile spidi gavana iliyowekwa itaondolewa na kweli mchakato huo utaendelea… hadi sasa sijaona wananchi wakielimishwa kuhusu Katiba kama ilivyoelezwa na wa-ziri. Hivyo, tukiendelea hivi, wananchi itafika mahali wataamua wenyewe,” amesema.
Kikwazo cha taasisi, ujumuishi
Mwandishi wa kitabu kilichozinduliwa, Dk Mandi ameelezea baadhi ya mambo ambayo yamo ndani ya kitabu hicho, akisema moja ya changamoto katika uundaji wa tume au taasisi za utunzi wa Katiba ni kutokuwapo mwafaka wa kitaifa kuhusu nani wanapaswa kuteuliwa.
“Ni muhimu tume ziundwe kwa ushiri-kishwaji mpana wa Serikali, chama ta-wala, vyama vya upinzani na asasi za ki-raia. Lazima ziwe taasisi zinazokubalika na kila upande, ili mapendekezo yake yawe na uhalali wa kitaifa,” amesema.
Vilevile ameeleza umuhimu wa kuwa na uwakilishi mpana wa makundi mbalimbali, wakiwamo wanawake, vijana, wanasheria, wanasiasa na wataalamu wa uchumi ili rasimu ya Katiba iwe jumuishi na kuakisi masilahi mapana ya Taifa.
“Tumeona kuwa ni muhimu katika kuun-da hizi taasisi kama tume, kuwe na mwafaka kwenye makundi yote; Serikali, chama tawala, vyama vya upinzani na asasi za kiraia. Lazima inapoundwa wote waiamini waseme hiki ni chombo am-bacho kimeundwa kutufanyia wote kazi kwa kuleta mapendekezo ambayo ya-naakisi masilahi mapana ya Taifa,” amesema.
Pia, amesema kitabu kinaeleza taasisi hizo zinahitaji kuangalia masilahi mapana na kuandika Katiba ambayo wananchi wote wataafiki kwamba hii ndiyo Katiba ya nchi yetu na si kufanya kwa lengo la kuwafurahisha watu wachache.
“Katika uteuzi wa tume, lazima kuwepo na ujumuishi kwa kuwa na watu wenye utaalamu mbalimbali, wanasheria, wanasiasa, wawakilishi wa wanawake, wawakilishi wa vijana, wataalamu wa uchumi. Lazima kuwepo na watu watakaoweza kuona kwa njia tofauti kwa sababu Katiba inatakiwa kuakisi mambo mengi mapana ya nchi,” amesema.
Profesa Gamaliel Mgongo-Fimbo, ames-ema moja ya changamoto kuu ni masi-lahi binafsi ya walioteuliwa katika tume na mabaraza ya katiba. Amesema wananchi wanapaswa kuviunga mkono vyama na makundi yenye dhamira ya kweli ya kudai Katiba mpya, badala ya kubaki watazamaji.
“Lazima tuanze kwenye uraia huku kwa support (kuunga mkono) vyama vya siasa au makundi yenye uelekeo wa kusaidia wananchi kupata Katiba. Hii ndiyo njia pekee ya kuwashinda wenye masilahi binafsi,” amesema.
Kwa upande wake, Profesa Chris Maina Peter amezungumzia umuhimu wa elimu ya Katiba, akitaka kitabu cha Dk Mandi kitafsiriwe kwa Kiswahili ili wananchi wengi wanufaike.
“Katiba ni mkataba kati ya wananchi na watawala. Lazima mtawala ajue kuwa utawala wake una kipimo, na kipimo hicho kipo kwenye Katiba. Tunahitaji Katiba nzuri kwa ajili ya Watanzania wote,” amesema.
Dk Rose Reuben amesema tafiti nyingi za wanataaluma zinahitaji kuufikia umma ili waweze kuzisoma.
“Kwa kufanya hivi maarifa ya kutoka kwa waandishi yanaweza kuchochea mjadala kidogokidogo ili kutakapoanza mchakato wa Katiba wawe wameshapata elimu ya kutosha,” amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba kuna taswira moja kuu: “Mkwamo wa Katiba mpya si kwa sababu ya kukosekana kwa mapendekezo au michakato, bali ni ukosefu wa utashi wa kisiasa, masilahi binafsi ya viongozi na uundaji wa taasisi zisizoakisi matakwa ya wananchi.”
Kwa maoni yake, iwapo kutakuwa na maridhiano ya dhati na dhamira ya kisiasa, Tanzania inaweza kupata Katiba mpya ndani ya mwaka mmoja.
“Vinginevyo, mchakato unaweza kuen-delea kukwama na mustakabali wa Taifa kuingia kwenye mashaka makubwa,” amesema.
Mchakato wa Katiba mpya uliokwama mwaka 2014 ulianza mwaka 2011 kwa utungwaji wa sheria za kuratibu na kusimamia utekelezaji wa upatikanaji wake.
Hizi ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83/2011 iliyoelekeza kuundwa vyombo vya kuratibu mchakato wa Kati-ba, yaani Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba (BMK) na Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11/2013.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili-yoongozwa na Jaji Warioba iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba iliyohaririwa na Mabaraza ya Katiba na kupata Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa kwenye BMK.
Katika Bunge hilo ambalo licha ya mvu-tano wa kiitikadi wa wajumbe uliosaba-bisha baadhi ya wajumbe kususia majadiliano na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lilijadili na Oktoba 2, 2014 lilipitisha Katiba Inayopendekezwa.
Oktoba 8, 2014, aliyekuwa Mwenyekiti wa BMK, Samuel Sitta aliikabidhi Katiba Inayopendekezwa kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, ambayo ilizinduliwa siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine ikiwemo kura ya maoni, ambazo hazikuendelea hadi leo.