Dk Msolla ashindwa kuvumilia, atoa tano kwa kina Hersi

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mbete Mshindo Msolla, ameshindwa kuvumilia na kuumwagia pongezi uongozi wa timu hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi sasa, huku akiwaomba wanachama kuendelea kushikamana kwa ajili ya mafanikio zaidi.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Yanga unaofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome Masaki, Dk Msolla amesema siri ya timu hiyo kufanya vizuri ni mshikamano unaoendelea baina ya wanachama wa kikosi hicho.

“Niwashukuru uongozi uliopo madarakani kwa sasa kwa kutupa heshima kubwa ya kuwepo hapa, jambo ambalo ninawasihi wanachama wenzangu ni kushikamana na kulipa ada ili timu yetu ifanye vizuri,” amesema Msolla kocha wa zamani wa klabu kadhaa na timu ya taifa, mbali na kuongoza kama Mwenyekiti wa klabu hiyo kabla ya kumpisha Injinia Hersi Said.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, inafanya mkutano wake mkuu leo kwa mujibu wa ibara ya 20 ya klabu hiyo ya mwaka 2021 ukiwa na ajenda 10, lakini ikiweka rekodi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu minne mfululizo.

Msimu uliopita pia ilitwaa Kombe la Muungano, Ngao ya Jamii na Toyota la Afrika Kusini, lakini ikifanikiwa kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili mfululizo iliyopita ikiwamo ile waliotolewa robo fainali na Mamelodi Sundowns mbali na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa kanuni ya vao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Awali Yanga ilipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 na kisha kwenda kushinda ugenini kwa bao 1-0 lililofungwa kwa penalti ya beki Djuma Shaaban na matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, lakini Waalgeria walitwaa kwa faida ya bao la ugenini. Kabla ya hapo Yanga ilikuwa haijawahi kufika hatua kama hiyo katika michuano ya CAF tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza 1969.