Wananchi watahamaki kupatwa kwa mwezi Dar

Dar es Salaam. Jana, Jumapili Septemba 7, 2025, Tanzania ilishuhudia tukio adimu la kupatwa kwa mwezi ambalo limeacha simulizi tofauti miongoni mwa wananchi.

Wakati baadhi ya makundi yalionekana kujikusanya mitaani kushuhudia kwa mshangao anga likibadilika na mwezi kufunikwa kwa kivuli cha dunia, wengine walihisi hofu kubwa na kujifungia ndani kwa imani kuwa ni ishara ya mabaya yanayoweza kutokea.

Katika maeneo kadhaa ya Dar es Salaam, wananchi walionekana wakishangaa anga lilivyogeuka taratibu, huku wengine wakipiga picha na video kupitia simu zao ili kukumbuka tukio hilo.

Hata hivyo, kulikuwa na kundi jingine lililodhani kwamba tukio hilo linaweza kuashiria maafa au laana kutokana na mitazamo yao, hivyo wakaanza kutafuta faraja kwa kujifungia kusali na kuomba dua.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wananchi walieleza walivyoshuhudia kwa hofu tukio hilo:

“Tulikuwa ndani, baada ya kutoka nje tuliona mwezi umefunikwa kabisa, ikawa giza kabisa na mwezi kuwa mwekundu.

“Kwakweli mimi nilihisi hofu, nikafunga mlango na kuomba, maana sijawahi kushuhudia jambo kama hili,” amesema mama mmoja (jina limehifadhiwa), mkazi wa Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati wengine wakihamaki na kushindwa kuvumilia, kwa upande mwingine, vijana walionekana kutumia tukio hilo kama fursa ya kuburudika, wakikusanyika kwa makundi kutazama kwa mshangao na kupiga picha tukio zima. Wengine walitumia tukio hilo kuthibitisha yale wanayojifunza shuleni kuhusu elimu ya anga katika somo la jiografia.

“Ni mara ya kwanza kuona mwezi unafunikwa kiasi hiki, nilifurahi kwa sababu najua ni sayansi ya kawaida, tumefundishwa darasani, si jambo la kuogopa,” alisema Mariam Said, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam.

Wataalamu wa astronomia, wakiwemo Brian Cox, mwanafizikia na mwanaastronomia maarufu kutoka Uingereza, na Jim Bell, Profesa wa astronomia kutoka Marekani, kupitia machapisho yao mbalimbali juu ya elimu ya anga, wanafafanua kupatwa kwa mwezi kuwa ni tukio linalotokea wakati dunia inapopita kati ya jua na mwezi, na kivuli cha dunia kufunika uso wa mwezi.

Kwa mujibu wao, tukio hili si hatari kwa binadamu, wanyama wala mimea, bali ni mzunguko wa kawaida wa anga unaotokea mara kadhaa kila mwaka katika sehemu mbalimbali duniani.

Wanaeleza kuwa kupatwa kwa mwezi hugawanyika katika aina kuu tatu: “kupatwa kamili,” ambapo mwezi hufunikwa kabisa na kivuli cha dunia; “kupatwa sehemu,” ambapo ni sehemu tu ya mwezi inayofunikwa; na “kupatwa kwa penumbra,” ambapo kivuli cha dunia hugusa kwa mbali na kufanya mwezi kuonekana wenye mwanga hafifu.

Kwa mujibu wa wasomi hao wa sayansi ya dunia, wanaonesha kuwa ni imani potofu kuhusisha kupatwa kwa mwezi na fikra za mikosi, maafa au janga lolote kuikumba dunia. Badala yake, wanahimiza tukio kama hilo litumike kuhamasisha elimu ya sayansi kwa watoto na vijana, na kuongeza ari ya utafiti kuhusu anga.

Awali, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikitoa taarifa kwa umma juu ya tukio hilo la kupatwa kwa mwezi, Septemba 6, 2025, ilisema wazi kuwa kupatwa kwa mwezi ni tukio linalotokea wakati dunia inapita kati ya jua na mwezi na kusababisha kivuli cha dunia kuwa katika uso wa mwezi.

“Tukio la kupatwa kwa mwezi kwa tarehe 7 Septemba 2025 ni la kupatwa kwa mwezi sehemu na kikamilifu. Tukio hili linatarajiwa kuonekana katika maeneo ya bara la Ulaya, Asia, Australia na Afrika.

“Kwa hapa nchini, hali ya kupatwa kwa mwezi inatarajiwa kuanza kwa kupatwa kwa mwezi sehemu kuanzia pale jua linapozama hadi saa 2:29 usiku na kufuatiwa na kupatwa kwa mwezi kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku,” ilifafanua taarifa hiyo siku moja kabla ya tukio lenyewe.

Kwa ujumla, tukio la jana limeacha funzo kubwa kwa taifa kuhusu haja ya elimu ya sayansi kuenea zaidi, ili jamii iondokane na hofu zisizo za lazima na badala yake ionekane ikifurahia maajabu ya dunia kwa uelewa mpana.