Dar es Salaam. Serikali ya Norway imeingia makubaliano ya miaka mitatu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mpango kazi wa miaka sita wa taasisi hiyo, unaolenga kuimarisha masuala ya haki za binadamu nchini.
Mpango huo wa LHRC wa mwaka 2025-2030 unalenga kuimarisha utawala wa kidemokrasia, haki na usawa kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Serikali ya Norway itashirikiana na taasisi hiyo kwa miaka mitatu.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo yaliyofanyika leo Jumatatu, Septemba 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes amesema ili kujenga jamii yenye haki, amani na usawa sambamba na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), kuna umuhimu wa Serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Tinnes amesema msaada huo una thamani ya takribani Sh4.5 bilioni na kupongeza LHRC kwa mchango wake katika kusukuma ajenda ya mabadiliko nchini kupitia utetezi, kesi za kimkakati na msaada wa kisheria.
“Norway imepiga hatua kubwa katika kujenga Taifa lenye amani. Ndiyo maana tunaunga mkono LHRC, kwa sababu wao wanaelewa vyema namna ya kujenga jamii ya Kitanzania yenye usawa,” amesema Tinnes.
Aidha, amesema LHRC imekuwa mstari wa mbele kuratibu mapendekezo ya asasi za kiraia kwa Serikali wakati wa vikao vya Umoja wa Mataifa vya Mapitio ya Mara kwa Mara ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) na inatarajiwa kushiriki tena mwaka 2026.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Fulgence Massawe amesema makubaliano hayo yamefikiwa kwa wakati muafaka.
Amesema yanakwenda kuchangia kujenga jamii yenye maridhiano ya kisiasa, uwezeshaji wa wanawake na uhuru wa kujieleza, kama nguzo muhimu za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Uimarishaji wa demokrasia si safari ya siku moja, bali unahitaji imani, ushiriki na dhamira ya wananchi pamoja na viongozi. Na kupitia sauti na maamuzi ya wananchi ndipo jamii hupata nguvu,” amesema Massawe.
Amesisitiza kuwa, demokrasia si haki ya kupiga kura pekee, bali ni pamoja na haki ya kuishi kwa amani, usalama na heshima.
“Ni kuhusu kujenga jamii ambayo wananchi wanaweza kutumia uwezo wao kikamilifu huku kodi zao zikielekezwa kwenye mahitaji muhimu kama elimu, afya, maji na miundombinu ya usafiri,” ameongeza.