TPA yaja na mkakati wa soko la DRC

Dar es Salaam. Baada ya mkakati wa maboresho kuongeza ufanisi wa utendaji wake, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) sasa imegeukia kuyasaka masoko, ikianza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

DRC inachangia zaidi ya asilimia 40 ya mizigo yote inayosafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, kwa mujibu wa ripoti ya TPA ya mwaka 2023.

Mamlaka hiyo imetuma ujumbe wa wataalamu wa masoko kutembelea DRC kwa ajili ya kuzungumza na wateja na kutatua changamoto zinazowakabili katika huduma za bandari za Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TPA, ujumbe huo umehusisha pia wataalamu kutoka kampuni za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, zikiwamo DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Lubumbashi, Magubilo Muroba, amesema ni muhimu kuwepo ushirikiano kati ya Tanzania na DRC ili kutanua zaidi soko hilo.

Amesema ushirikiano uliopo sasa umechangia ongezeko la shehena mwaka hadi mwaka. Takwimu zinaonesha ongezeko la asilimia 43 la shehena kutoka DRC, kutoka tani milioni 4.1 mwaka 2023/2024 hadi tani milioni 5.9 mwaka 2024/2025.

“Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza menejimenti ya TPA na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kushirikiana vyema na wafanyabiashara kutoka DRC, kwani ushirikiano huo ndio umechangia kukua kwa biashara ya mizigo inayopita katika bandari hiyo,” amesema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Josephat Lukindo, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa zaidi kwa uhusiano wa kibiashara uliopo.

Aidha, amesema lengo lingine la ziara hiyo ni kuwasilisha taarifa za mikakati na maboresho yaliyofanyika katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, na Kigoma, ili kuhakikisha huduma bora na ufanisi.

Amesema ushirikiano wa kiundeshaji uliopo kati ya TPA, DP World na TEAGTL, ununuzi wa mitambo ya kisasa uliofanywa na waendeshaji, na maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia TPA, yameongeza ufanisi.

Ameeleza kuwa kwa sasa muda wa kuhudumia meli za makasha umepungua hadi kufikia wastani wa siku tatu pekee.

Mbali na mkutano huo, ujumbe huo pia ulitembelea kampuni ya Impala Cargo Terminal nchini humo, ambayo ndiyo wasafirishaji wakubwa wa madini ya shaba na sulphur kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rik Matondo, ameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na bandari za Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara.

Kwa upande wa Kampuni ya Conexas Terminal, menejimenti yake imepongeza jitihada za TPA na waendeshaji wake, kwani wanaridhishwa na huduma zinazotolewa.