JKU yang’olewa kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika

Yei Joint Stars ya Sudan Kusini imeanza kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya JKU ya Zanzibar kwenye mechi ya kwanza ya kundi C la michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ulinzi Complex, Nairobi, Kenya.

Matokeo hayo yanaifanya JKU kuondolewa kwenye mashindano hayo ya Cecafa kwa Wanawake kutokana na vipigo viwili mfululizo kwenye hatua ya makundi dhidi ya JKT Queens 5-0 na Yei 4-2.

JKU ilianza kwa kasi  kwa kufunga mabao mawili ya haraka. Winfrida Mathias alifungua ukurasa wa mabao dakika ya kwanza kabla ya kuipatia timu yake bao la pili dakika mbili baadaye kufuatia uzembe wa safu ya ulinzi ya wapinzani, jambo lililoifanya Yei kuwa kwenye wakati mgumu.

Licha ya kuanza kwa kusuasua, Yei ilipunguza presha na kurejea na ari kubwa ya kutafuta matokeo na dakika ya 34 Aluka Grace alifunga bao la  na kuipa matumaini kabla ya mapumziko JKU ikiwa mbele kwa 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini JKU ilipoteza nafasi nyingi ilizozipata. Yei ilitumia vyema upungufu huo Ambayo Immaculate alisawazisha bao kabla ya Mariam Luis Lasuba kuongeza la tatu na kuifanya Yei iongoze 3-2.

Yei ilicheza kwa akili kubwa ikipunguza kasi ya mchezo na kudhibiti presha. Ushindi wake ulithibitishwa mwishoni ilipopata msaada wa bao la nne la kujifunga kutoka kwa JKU.

Mechi nyingine ya mapema iliyopigwa uwanjani hapo kati ya Rayon Sports dhidi ya Top Girls iliishw kwa suluhu.

Matokeo hayo yanaifanya Rayon kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake  baada ya kukusanya pointi nne.