HAIISHI hadi iishe. Ni neno unaloweza kutumia kuelezea ugumu wa kumpata bingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mbeya baada ya Flames na Tigers kutoshana nguvu katika mechi mbili za fainali.
Iko hivi, katika mchezo wa fainali ya kwanza iliyopigwa juzi Jumamosi, Flames iliibuka na ushindi wa pointi 88-62 dhidi ya wapinzani wao, ambapo fainali ya pili iliyochezwa jana Jumapili bingwa huyo mtetezi alihitaji ushindi ili kutetea taji.
Hata hivyo, hesabu zilionekana kwenda tofauti baada ya Tigers kuonyesha umwamba na kushinda mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani na mvuto ndani na nje ya uwanja kwa kutakata kwa pointi 66-59.
Kufuatia matokeo hayo, timu hizo zinararajia kukutana tena Jumamosi, wiki ijayo katika Uwanja wa Youth Centre jijini Mbeys kumpata bingwa wa ligi hiyo kwa mwaka huu na kuwakilisha ligi ya mabingwa wa mikoa nchini kwa mchezo huo.
Kocha wa Tigers, Peter Christopher amesema baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya kwanza walibaini makosa yao ambapo wachezaji wengi walikuwa na ugeni wa ligi hiyo na kukaa nao kuwapa mbinu namna ya kumaliza kibabe mchezo wa pili na kuweza kufanya kweli.
“Tunaenda kufanya maajabu Jumamosi ijayo, mashabiki wetu waje kwa wingi na tumejipanga mwaka huu kutwaa ubingwa huu, tunajua ugumu na umuhimu wa michuano hii,” ametamba kocha huyo.
Staa wa Flames, Humphrey George amesema wanakubaliana na matokeo hayo akieleza kuwa kilichowaangusha ni uchovu, akiahidi fainali ya tatu wiki ijayo timu hiyo haitakuwa na mzaha katika kutetea taji.
“Wachezaji hatujapoteza morali, lakini leo tukubali matokeo, vijana walichoka kwakuwa jana (juzi) tulitumia nguvu kubwa hivyo tunaenda kujipanga na mchezo wa mwisho ili kuendeleza heshima yetu katika ligi hii,” amesema George.
Mmoja wa wadau wa mchezo huo, Juverino Pembe amesema amekuwa akivutiwa na mchezo huo akibainisha kuwa Mbeya imekuwa na vipaji katika ligi ya Kikapu hadi kumfanya kutoa motisha ya zawadi kwa wachezaji bora kwa upande wa wanaume na wanawake.
“Nimesafiri kutoka Dar es Salaam kufuatilia fainali hii, kutokana na ushindani na mvuto bado bingwa hakupatikana lakini binafsi nimeamua kutoa zawadi kwa wachezaji bora kwa Wanawake na Wanaume ili kuongeza chachu zaidi.
“Niwaombe wadau wengine kutoa sapoti kwa mchezo huu ili kuendeleza na kuibua vipaji zaidi, Mbeya imekuwa na ligi bora yenye kuvutia tuungane kuwasapoti,” amesema mdau huyo.