Taifa Stars v Niger Mechi ya hesabu

KIKOSI cha timu ya taifa, Taifa Stars jioni ya leo kinatarajia kushuka kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuikabili Niger ikiwa ni mechi ya hesabu za kuisaka tiketi ya kwenda katika Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Baada ya kukosa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki fainali hizo za mwakani kutokana na Morocco kuinasa mapema ikiongoza Kundi A, nafasi pekee kwa Stars inaweza kuipata ni kupitia hatua ya mchujo kwa kuanzia Kanda ya Afrika na kisha baadaye kidunia.

Na ili hilo la mchujo lifanikiwe, lazima ishinde leo mbele ya Niger ili ifikishe pointi 13 na kusaliwa na mechi moja mkononi dhidi ya Zambia ambayo ikipata ushindi itajihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili ya kundi E ikiwa na pointi 16.

Kwa Afrika, baada ya hatua ya makundi kumalizika, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeweka utaratibu wa kupunguza pointi kwa timu zote zilizopo makundi yenye timu sita ilizopata dhidi ya zilizoshika mkia kwa kila kundi ili kupata uwiano na timu zilizoshika nafasi ya pili kwa makundi yale yenye timu chache.

Tanzania ikimaliza nafasi ya pili iwapo itashinda mechi zote mbili zilizobakia dhidi ya Niger na Zambia itakazocheza nyumbani, itakuwa ni kati ya wanufaika kwa vile yenyewe haitopunguziwa pointi zake kwa vile kundi ililopo lina timu chache kulinganisha na mengi ambapo lina timu tano.

Kwa sasa timu nne zilizo juu katika chati ya zile zenye idadi kubwa ya pointi zilizoshika nafasi ya pili, Gabon ndio kinara ikiwa na pointi 17 ikifuatiwa na Cameroon yenye pointi 15 sawa na Senegal iliyo nafasi ya tatu na Burkina Faso inafuatia ikiwa kwa pointi 14.

Hata hivyo, Burkina Faso, Cameroon, Senegal na Gabon zote zipo makundi yenye timu sitasita kila moja kulinganisha na Taifa Stars ambayo ipo kundi lenye timu tano.

Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo, Stars ilishinda ugenini kwa bao 1-0, hali inayoipa nafasi ya kuendelea pale ilipoishia ili kutimiza lengo la kukata tiketi ya kwenda Marekani, Canada na Mexico.

Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema bado wana matumaini makubwa ya kupata nafasi ya kucheza mechi za mchujo.

“Hatujapata matokeo ambayo tuliyategemea dhidi ya Congo lakini pointi moja tuliyopata ni muhimu. Nafasi tunayo ya kucheza hatua ya mchujo kama tutashinda mechi mbili zilizobakia.

“Tutajitahidi kurekebisha upungufu uliojitokeza katika mechi ya Congo ili tufanye vizuri katika mchezo unaokuja dhidi ya Niger,” alisema Morocco.

Kumbukumbu zinaonyesha Stars imekuwa na historia nzuri katika michezo yake dhidi ya Niger ambapo katika mechi tatu walizokutana, imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja.

Pia Stars inaingia katika mechi ya leo ikiwa na mwenendo mzuri kulinganisha na wapinzani wao Niger.

Katika mechi sita zilizopita hivi karibuni, Taifa Stars imepata ushindi mara tatu, imetoka sare mbili na kupoteza moja tu. Niger katika mechi sita zilizopita haijapata ushindi na imetoka sare tatu huku ikipoteza mechi tatu.