Hawa ndio wapinzani wa ‘mnyama’ Simba Day

KATIKA kuhitimisha maandalizi ya msimu mpya, Simba itashuka dimbani leo, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili mabingwa wa kihistoria wa Kenya, Gor Mahia katika tamasha la Simba Day.

Mechi hiyo ya haitakuwa tu fursa kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kuwaona wachezaji wapya, bali ni kipimo cha kikosi hicho kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Septemba 16.

Gor Mahia FC ilianzishwa 1968 ikiwa ni matokeo ya muungano wa klabu mbili ambazo ni Luo Union na Luo Stars na mmoja wa wanzilishi alikuwa mwanasiasa Tom Mboya.

Tangu wakati huo timu hiyo ambayo a.k.a yake ni K’Ogalo imejijengea heshima kama klabu yenye mafanikio zaidi katika historia ya soka la Kenya na moja ya klabu zenye mashabiki wengi Afrika Mashariki kama zilivyo Simba na Yanga.

Mpaka sasa Gor Mahia imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya mara 21 ikishikilia rekodi ya juu zaidi katika historia ya soka la huko, imebeba mara nane Kombe la Ligi na tatu lile la Kagame.  Pia imeshiriki michuano mingi ya CAF na ni ya kwanza Kenya kutwaa taji la Kombe la CAF 1987.

Katika misimu ya karibuni, Gor Mahia imeonyesha ubora licha ya changamoto za kifedha na mabadiliko ya kiuongozi. Mwaka 2023 ilirejea kwenye ubora baada ya kuwa na misimu miwili migumu ikitwaa taji la 20 na uliofuata ikabeba la 21. Hata hivyo msimu uliopita ilizidiwa kete na Police inayonolewa na, Etienne Ndayiragije na kuishia kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 59 kwenye msimamo ikidiziwa pointi sita na maafande hao.

Kikosi cha sasa kina mchanganyiko wa vijana wenye vipaji pamoja na wachezaji wa kimataifa wenye uzoefu. Baadhi ya wachezaji hatari ni pamoja na Austin Odhiambo ambaye ni kiungo machachari na ni kati ya wachezaji wa timu ya taifa la Kenya ‘Harambee Stars’  ambao walifanya vizuri kwenye mashindano ya CHAN 2024.

Hii siyo mara ya kwanza Gor Mahia na Simba kukutana. Mechi za timu hizo zimekuwa na mvuto, kwani 2018 wababe hao walikutana mara ya mwisho katika fainali ya SportPesa Super Cup ambapo Simba ilichapwa 2-0 wafungaji wakiwa ni Meddie Kagere na Jacques Tuyisenge.

Baada ya mashindano hayo Simba ilimsajili Kagere ambaye alifanya makubwa akiwa na jezi ya Wekundu wa Msimbazi na kuweka rekodi kibao, ikiwemo kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo akifunga mabao 23 na 22 mtwalia. Hali ya ushindani kati ya timu hizo mbili ni kubwa kutokana na ukubwa wa kila moja. kwa Gor Mahia itakuwa ni nafasi ya kuendeleza kile ilichofanya mara ya mwisho na ikapata nafasi ya kwenda England kucheza dhidi ya Everton. Lakini kwa Simba itakuwa ni fursa ya kuonyesha ubabe wake Afrika Mashariki maana ndio klabu kinara kwa sasa kwa mujibu wa CAF ikishika nafasi ya tano kwa Afrika, huku Gor Mahia haipo kwenye orodha hiyo ya timu 75 bora ambayo ilitolewa mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Siku chache zilizopita Gor Mahia ilimteua Mghana Charles Kwabla Akonnor kuwa kocha mkuu mpya ambaye aliwahi kuchezea timu kadhaa Ulaya na pia nahodha wa timu ya taifa ya Ghana (Black Stars).