BAADA ya miaka saba kupita, hatimaye miamba ya soka la Tanzania na Kenya, Simba na Gor Mahia Zinakutana tena leo Jumatano katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki kwenye kilele cha Tamasha la Simba Day utakaochezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana, ilikuwa Juni 2018 na Simba ilipoteza huko Kenya kwa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia, ilikuwa ni katika fainali ya michuano ya SportPesa na mechi hiyo ndiyo iliyoifanya Simba kumsajili Meddie Kagere.
Kagere ambaye alikuwa kwenye kiwango bora, alifunga moja ya mabao yaliyoifanya Simba kukosa nafasi ya kwenda England kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Everton.
Beki wa kulia na wekundu hao wa Msimbazi, Shomary Kapombe ndiye mchezaji pekee aliyesalia katika kikosi hicho hadi leo na Simba itacheza mechi nyingine ya kimataifa dhidi ya Gor Mahia.
Katika historia ya michezo ya Simba Day kuanzia mwaka 2009 hadi 2024, Simba imeshinda jumla ya mechi 11 kati ya 16, ikiwemo dhidi ya SC Villa (2009, 2013 na 2015), AFC Leopards (2016), Rayon Sports (2017), Asante Kotoko (2018), Power Dynamos (2019 na 2023), Vital’O (2020), St George (2022) na APR (2024).
Imetoa sare mmoja pekee dhidi ya Express mwaka 2010, huku ikipoteza michezo minne dhidi ya Victors (2011), Nairobi City Stars (2012), Zesco United (2014) na TP Mazembe (2021).
Gor Mahia ambayo itakutana na Simba leo, imeshinda Ligi Kuu ya Kenya mara 21, hiyo ni rekodi ya juu zaidi na imeshinda Kombe la FKF mara 11, ambayo nayo ni rekodi.
Akizungumzia mechi hiyo ya kirafiki, Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema italeta ushindani kwa sababu Gor Mahia ni timu yenye historia kubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na itasaidia kupima maandalizi yao ya msimu ujao. “Tunawaheshimu Gor Mahia. Ni mechi ambayo mashabiki wataiona Simba mpya, yenye sura tofauti pia yenye roho ya Simba ileile. Hii ni mechi ya majaribio, lakini wachezaji wanajua ni lazima waonyeshe wapo tayari kwa msimu mpya,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa Gor Mahia, Charles Kwabla Akonnor alisema; “Hii ni mechi nzuri na muhimu katika maandalizi yetu ya msimu ujao, Simba ni timu nzuri hivyo tupo tayari kuwapa changamoto.”