Gamondi, Maximo uso kwa uso Kagame

KWA mara ya kwanza makocha, Marcio Maximo wa KMC na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars watakutana Ijumaa ya Septemba 12 katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Cecafa Kagame baada ya kila mmoja kutinga kibabe hatua hiyo.

Makocha hao wenye historia ya aina yake kwenye soka la Tanzania, wameziongoza klabu hizo za Tanzania kila mmoja kuvuna pointi saba, zikishinda mechi mbili na kutoa sare moja hivyo kumaliza hatua ya makundi na rekodi ya ushindi wa asilimia 66.7.

Singida BS ikiwa kundi A, ilianza mashindano hayo ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza kwa suluhu dhidi ya Ethiopian Coffee, ikaichapa Polisi ya Kenya inayonolewa na kocha wa zamani wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije mabao 2-1 na mechi yao ya mwisho ikaichapa Garde Cotes FC ya Djibout bao 1-0.

Kwa upande wa vijana wa Kinondoni, KMC ilianza kwa kuichapa mabingwa wa Ligi ya Zanzibar, Mlandege kwa mabao 3-2, ikaendeleza tena ubabe dhidi ya Bumamuru kwa bao 1-0 na kumaliza hatua hiyo kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya APR ya Rwanda.

Licha ya timu hizo za Ligi Kuu Bara kila moja kumaliza hatua hiyo akiwa na pointi saba katika makundi tofauti, Singida BS ikiwa A na KMC B, mmoja alimaliza akiwa kinara wa kundi lake na mwingine akishika nafasi ya pili.

KMC imemaliza ikiwa nafasi ya pili kundi B, licha ya kulingana pointi na APR ambao ni wanafainali ya michuano iliyopita, imezidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo kujikatia tiketi ya nusu fainali kwa mlango wa ‘best looser’.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu tatu zilizomaliza kinara wa kila kundi hufuzu hatua ya nusu fainali na kwa kuwa makundi yapo matatu, huwa tatu ili kukamilisha idadi ya timu nne na huchaguliwa moja iliyofanya vizuri zaidi lakini haikumaliza kinara wa kundi lake, hiyo ndiyo njia ambayo KMC imepenyea.

Kwa mujibu wa ratiba, kinara wa kundi A ambayo ni Singida BS ndiyo itacheza dhidi ya best looser ambaye ni KMC iliyoizidi kete Polisi ya Kenya iliyokusanya pointi sita kwenye kundi A.

Mechi hiyo ya nusu fainali baina ya Singida BS dhidi ya KMC, itawakutanisha makocha ambao mmoja, Gamondi anarekodi ya kutwaa mataji matatu akiwa na Yanga, Ligi Kuu Bara 2023/2024 na ilikuwa taji 30 kwa timu hiyo ya Wananchi tangu mwaka 1965. Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii 2024.

Pia kocha huyo, aliandika historia kwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Kwa upande wa Maximo ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu za taifa za vijana wa Brazil (chini ya miaka 17 na chini ya miaka 20) kati ya mwaka 1992 na 1993, Juni 29, 2006 aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania.

Akiwa na Taifa Stars, aliweka historia kwa kuifanya Tanzania kwa mara ya kwanza kufuzu kwa fainali za CHAN zilizofanyika Ivory Coast kuanzia mwaka 2009 na ilifuzu baada ya kuiondoa Sudan kwa jumla ya mabao 5–2.

Hatma ya kundi C ambalo limetawaliwa na sare itafahamika leo, Jumatano na Mogadishu City itacheza dhidi ya Al-Ahly Wad Madani na Al-Hilal Omdurman itacheza dhidi ya Kator.

Al-Hilal Omdurman, Al-Ahly Wad Madani, Kator na Mogadishu City kila mmoja amejikusanyia pointi mbili dakika 180 alizocheza katika mechi mbili zilizopita za michuano hiyo.

Ikumbukwe timu hizo zilishindwa kutambiana kwa mara ya kwanza, Septemba 4 katika mechi zao za kwanza na Al-Hilal Omdurman ya Sudan ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mogadishu City ya Somalia huku Al-Ahly Wad Madani ya Sudan ikitoka suluhu dhidi ya Kator ya Sudan Kusini.

Katike mechi za Jumapili, Al-Hilal Omdurman ilibanwa mbavu na ndugu zao kutoka Sudan, Al-Ahly Wad Madani kwa sare ya bao 1-1 huku Kator ikiendelea kutoruhusu bao wala kufunga kwenye mashindano hayo kwa kutoa suluhu ya pili, safari hii ikiwa dhidi ya Mogadishu City.

Kwa matokeo hayo, kundi hilo linaongozwa na Al-Hilal Omdurman yenye mabao mawili ya kufunga na kufungwa, Al-Ahly Wad Madani inashika nafasi ya pili ikiwa na bao moja la kufunga na kufungwa sawa na Mogadishu City.

Kinara wa kundi hilo itacheza dhidi ya APR katika nusu fainali nyingine ya michuano hiyo mikogwe ambayo Rais wa Rwanda, Paul Kagame ametoa Dola 60,000 kwa ajili ya zawadi ambazo ni zaidi ya Sh162 milioni.