NIKWAMBIE MAMA: Ahadi zenu zisigeuzwe chachandu za kampeni

Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 zinazidi kupamba moto. Kila mgombea katika nafasi anayoipigania amekuwa akiongeza kasi inayoambatana na vionjo vipya kwenye ahadi zake. Kuna wanaoleta ucheshi, lakini wengi wao wamebeba mafurushi ya ahadi bila kujali utekelezekaji wake. Mgombea ataahidi lolote hata kabla hajajua nini mahitaji ya mahala husika, atajinadi kutokomeza changamoto hata kabla hajazisikia.

Tumesikia kila aina ya ahadi katika mikutano mbalimbali ya kampeni za mwaka huu. Katika kipindi hiki wagombea wanatumia changamoto za ujumla kutoa ahadi kwenye majimbo. Kila jimbo linaahidiwa barabara za kiwango cha lami, vituo vya afya, shule na miradi itakayotoa fursa za ajira kwa wakazi wa jimbo husika. Wakati huu kila jimbo ni muhimu zaidi ya majimbo yote.

Makundi makubwa yaliyosahaulika kwa muda mrefu, yamekuwa yakifikiwa zaidi na ahadi. Vijana wasio na ajira, kinamama wasio na uhakika wa uzazi salama na watoto wanaotembea mwendo mrefu kusaka elimu wamekuwa wakitajwa zaidi kwenye mshikemshike huu. Hili linadhihirisha kuwa changamoto za Watanzania zanajulikana, ila tatizo ni kukosekana kwa utatuzi wake.

Vijana wasio na ajira na waliojiajiri kwenye mifumo isiyo rasmi wamekuwa wakiahidiwa maisha bora na karibu kila mgombea. Baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wamefikia hatua ya kujipambanua kiitikadi baada ya kukolezwa na ahadi hizi. Hawa wanaahidiwa aidha kuvutwa Serikalini kwenye ajira rasmi, au kuboreshewa shughuli zao kila mmoja akipatiwa bodaboda yake na mtaji.

Wapo wanaosikiliza hadithi za wagombea kama wanaosikiliza muziki wa ala. Wanashangilia kila neno kulingana na utamu wake bila hamu ya kujua zaidi. Lakini walio wengi wanajiuliza ni miujiza gani itakayofanyika kufanikisha ahadi zilizoshindikana tangu enzi na enzi. Iwapo kila mmoja angepata nafasi ya kuhoji, sidhani kama wangemaliza msururu na pengine kura zingepigwa karne ijayo.

Faida na hasara katika mtindo huu wa kampeni zinafanana na ulevi. Mtu anaposongwa na deni anaweza kuamua kulewa ili kujisahaulisha tatizo hilo.

Lakini ulevi unapokwisha kichwani, tatizo huongezeka maradufu kwa sababu matumizi yasiyo ya lazima. Badala ya kupunguza deni, mlevi anaziteketeza pesa zake kirahisi kabisa. Na si ajabu akaishiwa hela za kulewea, akaongeza deni la pombe.

Wananchi wanaosikiliza kampeni wanaweza wakafurahishwa sana na ahadi za wagombea. Hii ni kwa sababu wameteseka sana na ubovu wa huduma za kijamii na gharama za maisha. Kwa mfano walisafiri kwa mwendo mrefu kutafuta matibabu. Lakini baada ya kuletewa huduma hiyo karibu, wanashindwa kukidhi gharama za matibabu. Wapendwa wao wanakufa kwa kushindwa kulipia gharama hizo.

Watu wa aina hii huwa na uchungu wa hali ya juu sana. Wanakuwa tayari kuuondoa uongozi ulio madarakani, lakini udhaifu wa wapinzani unawalazimisha kubaki walipo. Wagombea wote wanakuja na sera zilezile zilizokwisha kutajwa, kinachoongezeka kinafanana na matone ya mvua katikati ya bahari.

Hivi sasa Watanzania wana upeo mkubwa kulinganisha na zamani. Pamoja na kwamba hata wa zamani walikuwa hivyo, lakini wa sasa wanajua zaidi kupitia teknolojia. Hivi sasa habari zipo kwenye mitandao ya kijamii iliyo mingi kuliko wanayoifahamu, tofauti na wakati ule wa magazeti ya chama na Serikali. Wanapata elimu na mifano mingi ya kampeni na chaguzi kutoka duniani kote.

Nawaasa wagombea waache kutoa ahadi zisizotekelezeka. Waelewe kuwa wanasikilizwa na wapigakura wenye akili timamu na uelewa wa kutosha. Hivi leo mgombea yeyote ana haki ya kutoa ahadi za “danganya toto” bila hofu yoyote. Bahati yao kuwa bado wapiga kura hawajaipata ile haki ya kuwashtaki pale wanaposhindwa kutimiza ahadi, vinginevyo tusingesikia bla-bla tunazozisikia.

Lakini vijana wakatae kutumika kama chambo katika kampeni. Uhaba wa ajira hauondoi sifa hiyo pamoja na kuwa ni tatizo la kiulimwengu. Wadai elimu itakayowawezesha kujiajiri. Wana haki ya kujua ni vipi watajengewa uwezo wa kuingiza kipato cha kukidhi maisha yao, badala ya kusubiri ndoto za maisha bora kupitia huduma za bure.

Wananchi wanaombwa kura kwa ahadi za kupewa elimu na matibabu bila malipo. Hawaelezwi huduma hizo zitagharamiwa na nani. Nionavyo mimi, ni Serikali ndiyo itakayolazimika kugharamia au kutoa ruzuku kwenye huduma hizo na nyingine za msingi. Swali ni je, Serikali imeandaa fungu kwa ajili hiyo? Hata kama chama kipya kitafuzu kuunda Serikali, je, kitazikuta fedha za kugawa ruzuku?

Wananchi waambiwe ukweli kuwa huduma za bure zinaweza kupelekea ongezeko la kodi. Kodi zitapanda ili kuongeza pato la Serikali litakaloiwezesha kumudu kuwahudumia.

Wasipoona kodi za mapato zikipanda, wataona gharama zikipanda kwenye manunuzi na huduma. Watanunua bidhaa kwa bei ghali na maisha yatakuwa magumu kuliko kulipia huduma kwa kuchangia.

Si vibaya kwa wagombea kuweka malengo yao ya kabla hadharani. Lakini ingelikuwa bora zaidi wangefanya utafiti wa jinsi fedha zinavyopatikana na kutumika. Naamini wananchi wataelewa vizuri iwapo watapewa ahadi kwa kupitia michanganuo rahisi.