SIMBA DAY: Nje moto ndani moto

UMEUONA mziki wa Simba SC? Najua hujauona vizuri, sasa Septemba 10, 2025, vyuma vyote vinawekwa hadharani kwa kutambulishwa mbele ya mashabiki kisha utapigwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia kutoka Kenya.

Hiyo itakuwa ni kilele cha Tamasha la Simba Day ambalo mwaka huu ni msimu wa 17 linakwenda kufanyika. Uwanja wa Benjamin Mkapa, utapambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe kunogesha shughuli hiyo.

Katika kikosi cha Simba, kuna sura mpya 12 zilizosajiliwa kipindi cha dirisha kubwa lililofunguliwa Julai Mosi, 2025 na kufungwa Septemba 7, 2025.

BURU 01


Wachezaji hao ni Yakoub Suleiman kutoka JKT Tanzania, Naby Camara, Antony Mligo (Namungo), Rushine De Reuck (Mamelodi Sundowns), Wilson Nangu (JKT Tanzania), Alassane Kante (Club Athletique Bizertin), Morice Abraham (mchezaji huru), Mohammed Bajaber (Police Kenya), Hussein Semfuko (Coastal Union), Jonathan Sowah (Singida Black Stars), Seleman Mwalimu (Wydad Casablanca) na Neo Maema (Mamelodi Sundowns).

Nyota hao wapya wanaungana na wale waliobaki baada ya kuondoka kwa Aishi Manula, Mohamed Hussein, Omary Omary, Fabrice Ngoma, Valentine Nouma, Hussein Kazi, Augustine Okejepha, Kelvin Kijili, Debora Mavambo, Fondoh Che Malone, Edwin Balua na Leonel Ateba.

Baada ya usajili kufungwa chama la Simba limeonekana kuwa na kikosi kipana kinachompa kocha Fadlu Davids uhuru wa kuandaa timu ya ushindi kulingana na mpinzani wa siku husika.

Kumbuka Simba iliyoweka kambi Misri kabla ya kurejea Dar es Salaam kumalizia maandalizi, ilicheza mechi tano za kirafiki ikishinda tatu, sare moja na kupoteza moja.

BURU 02


Matokeo ya mechi hizo yalikuwa hivi; Simba 2-0 Kahraba Ismailia, Simba 3-4 ENPPI, Simba 1-0 Al Zulfi, Simba 2-0 Wadi Degla na Simba 1-1 FC Fassell.

Hapa Mwanaspoti linakuwekea upana wa kikosi cha Simba SC ulivyo kulingana na nyota wapya na wale waliobaki kuipambania timu hiyo.

BURU 05


Hilo ndilo jeshi ambalo unaweza kusema la mauaji ambapo golini anakaa Moussa Camara, beki wa kulia Shomari Kapombe na kushoto Naby Camara mwenye uwezo pia wa kucheza kiungo mkabaji. Mabeki wa kati ni Rushine De Reuck na Chamou Karaboue, huku Yusuph Kagoma akiwa kiungo wa chini na kiungo wa juu Mohamed Bajaber.

Kibu Denis ni winga wa kulia na kushoto ni nafasi ya Elie Mpanzu. Mshambuliaji wa mwisho Jonathan Sowah na Jean Charles Ahoua akicheza namba kumi.

BURU 04


Kipa anakaa Yakoub Suleiman, beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ na kushoto Antony Mligo. Mabeki wa kati Wilson Nangu na Abdulrazack Hamza, Alasane Kante akicheza kiungo wa chini.

Winga ya kulia unamkuta Joshua Mutale na kushoto Ladack Chasambi. Kiungo wa juu Semfuko Charles, Seleman Mwalimu ni mshambuliaji wa mwisho akipigwa tafu na Neo Maema.