Bado Watatu – 24 | Mwanaspoti

Hata kama nitaendelea kuificha maiti ya Shefa, mtu aliyemuua atakuwa anajua kuwa maiti ya Shefa nimeificha humu ndani. Kama ataamua kunisaliti, anaweza kuwatonya polisi wakaja wakapekua nyumba yangu na kuikuta.

Mawazo yote hayo yalipita katika akili yangu na kunikatisha tamaa. Niliona kwamba muda wangu wa kukamatwa na kuhusishwa na mauaji yale ulikuwa karibu sana.

Kwanza, sikujua mwili huo wa Shefa ambao ulikuwa ni kidhibiti kikubwa cha kunitia katika hatia ningeuhamishaje pale nyumbani bila kuonekana. Na hata kama ningeweza kuuhamisha, nilijiuliza tena, nitaupeleka wapi?

Lilikuwa ni jambo lisilowezekana kuendelea kuufungia mwili huo katika chumba hicho cha stoo huku ukiendelea kuharibika na kutoa harufu.

Mume wangu atakapokuja nitamwambia nini? Nilijiuliza.

Niliingia chumbani nikakaa kitandani. Ghafla nikakumbuka kitu ambacho kilinishitua sana. Nililikumbuka lile gari la Shefa ambalo aliliegesha usiku kabla ya kuja kwangu.

Nikaondoka pale kitandani na kwenda kufungua dirisha. Nikapenua pazia na kulichungulia gari hilo. Nikaliona. Nikajiambia, kama gari hilo litaonekana litakuwa ni ushahidi kuwa Shefa alikuja kwangu.

Nitafanya nini jamani mie? Nilijiuliza kwa uchungu.

Hapo hapo nikapata wazo kwamba nikimbie. Nikajiuliza nitakimbilia wapi? Akili ilinituma nikimbilie nyumbani kwetu Sahare au Dar.

Lakini nikajiambia, kama maiti ya Shefa itakutwa nyumbani kwangu, hata nikimbilie wapi nitakamatwa tu.

Na hata kama nitajitetea kwa kueleza ukweli uliotokea, bado nitakabiliwa na shtaka la mauaji kutokana na kutoueleza ukweli huo mapema.

Nikaona kukimbia halikuwa wazo la maana. Nikikimbia ndiyo nitadhihirisha kuwa mimi ndiye niliyemuua Shefa.

Baada ya kuona wazo la kukimbia halifai, nikapata wazo jingine kwamba nijipeleke polisi mwenyewe, nikawaeleze ukweli uliotokea. Lakini niwe tayari kupewa talaka na Sufiani na pia niwe tayari kuwekwa ndani hata kwa miaka miwili kupisha uchunguzi.

Nikajikuta siko tayari kupewa talaka kirahisi, na pia sikuwa tayari kuwekwa ndani kwa muda wote huo. Nilikuwa na hakika iwapo nitawekwa ndani katika kipindi hicho nitafia huko huko jela.

Ilikuwa wazi kuwa lile tukio lilisababisha nirukwe na akili, kwani sikukumbuka kuchemsha chai wala sikukumbuka wajibu wangu mwingine zaidi ya kuwaza tu.

Kazi yangu ilikuwa ni kukaa kisha kuanza kurandaranda humo ndani. Kila wakati nilikuwa ninafungua mlango wa stoo na kuutazama mwili wa Shefa kwa tamaa kwamba huenda amezinduka.

Ilipofika saa nne hivi nikasikia mlango unabishwa. Nikajiuliza, ni nani? Baada ya kusita kidogo nikaenda kuufungua. Nikashituka nilipomuona mke wa Shefa.

“Karibu,” nikamwambia huku nikimtazama kwa macho ya tashwishi. Laiti angekuwa mwanasaikolojia, mara moja angegundua kuwa ujio wake ulikuwa umenishitua.

Sasa angejiuliza, kwa nini nimeshituka wakati kuna tukio la kupotea kwa mumewe?

Mwanamke huyo, aliyenizidi makamo kidogo, aliingia ndani baada ya kumpisha kwenye mlango.

“Vipi, umefanikiwa kumpata mumeo?” nikajidai kumuuliza huku jicho langu likimulika mlango wa stoo ulimokuwa mwili wa mume wake.

“Hivi unavyoniona natoka hospitali ya Bombo. Pale nilipokupigia simu, polisi walikuja nyumbani kumtafuta mume wangu.”

“Polisi wanamtafuta kwa ajili gani?” nikamuuliza.

Wakati huo tulikuwa tumesimama kando ya mlango karibu kabisa na mlango wa ile stoo.

“Wameniambia lori lake limepinduka usiku wakati linatoka Mombasa. Dereva amefariki na taniboi wake yuko mahututi. Wakaniambia kwamba hao watu wameshapelekwa hospitali ya Bombo, yaani huyo taniboi na huyo dereva aliyekufa.”

“Mmh… makubwa… sasa ndiyo umekwenda huko Bombo?”

“Nimekwenda nikidhani labda mmojawapo alikuwa Shefa. Wale polisi hawamjui Shefa kwa sura. Lakini nilipokwenda kuwatazama, Shefa hakuwepo. Anatakiwa aende kituo cha polisi cha Chumbageni. Imegundulika kuwa lori lake hakulikatia bima.”

“Ni makubwa kidogo dada! Wala usiseme! Pale mwanzo namba yake ilikuwa inapatikana, lakini kwa sasa ukiipiga simu haiiti tena. Sasa sijui amekimbia baada ya kusikia anatafutwa na polisi?”

“Inawezekana,” nilisema, lakini sauti yangu haikuwa na nguvu.

“Sasa kwa nini asinifahamishe angalau kwa meseji?”

“Labda mwenzako amechanganyikiwa, hajui afanye nini.”

“Sidhani. Hii si tabia yake. Nimepitia tu hapa kwako kukufahamisha hali ilivyo, narudi nyumbani. Hata chai sijakunywa kwa fadhaa.”

“Pole dada kwa misukosuko. Ukifika bandika chai unywe. Mume wako atakuja tu.”

“Na hiyo kesi inayomngoja itakuwaje? Lori halina bima?”

“Si atalipa faini tu.”

“Ni mpaka awe nayo hiyo pesa, kama hana itakuwaje? Si anakwenda kufungwa?”

“Sidhani kama atakosa.”

“Lori lenyewe ndiyo hilo limeshapinduka, kuna pesa tena?”

“Muhimu ni yeye kupatikana.”

Mwanamke huyo akageuka na kuniambia:
“Kwaheri.”

“Karibu dada… basi tufahamishane litakalotokea.”

Wakati mwanamke huyo anatoka, nikalikumbuka lile gari la Shefa aliloliegesha usiku. Nilihofia angeweza kuliona na kulitambua. Nikamchungulia kwenye mlango. Kwa bahati njema hakuelekea upande ule, alielekea upande mwingine.

Hata hivyo, nilijiambia, gari hilo litakuja kuonekana tu. Ningekuwa na uwezo wa kuliondoa ningeliondoa na kulipeleka mtaa mwingine.

Nikafunga mlango na kufungua mlango wa stoo. Nilipapasa mifuko ya Shefa nikatoa funguo za lile gari. Nilipanga kuangalia uwezekano wa kwenda kuliondoa gari hilo na kwenda kuliegesha mtaa mwingine.

Nilizichukua zile funguo na kutoka katika kile chumba. Nikafunga mlango na kwenda sebuleni. Niliziweka funguo hizo kwenye kochi na mimi nikakaa hapo hapo.

Hapo nikawa nafikiria nitakavyoweza kwenda kuliondoa gari la Shefa. Nikajiambia, kwa vile nitakuwa na funguo za gari hilo, niende pale nifungue mlango wa gari hilo na kujipakia.

Kwa kuwa mlinzi aliyekuwepo usiku, ambaye alimuona Shefa, atakuwa hayupo tena, hakutakuwa na mtu yeyote atakayeniuliza kuhusu gari hilo. Kila atakayeniona atajua kuwa linanihusu.

Niliendelea kujiambia, nitakapoondoka nalo nitakwenda kutafuta mahali pengine katika mtaa mwingine niliegeshe.

Nilikuwa na wasiwasi kwamba gari hilo likiendelea kuwa mahali alipoliacha Shefa, litanizushia tuhuma mimi, hasa kwa vile aliyemuua Shefa atakuwa anajua kuwa Shefa alikuja kwangu na gari lake aliliacha pale.

Wakati ninawaza hivyo, nikasikia mlango wa nje unagongwa. Moyo wangu ukashituka. Kila kitu sasa kilikuwa kikinishitua moyo. Sikujua ni nani aliyekuwa anabisha, labda ni polisi au mke wa Shefa amerudi baada ya kuona gari la mume wake mahali alipoliegesha!

Nikainuka na kwenda kufungua mlango. Alikuwa shoga yangu Raisa!

“Bado uko nyumbani tu?” akaniuliza alipoingia ndani.

“Sijatoka shoga. Nilikuwa namalizia vijikazi vya nyumbani. Umefika kule saluni?”

“Nimefika nikaambiwa hujakuja.”

“Si ungetengenezwa tu shoga.”

“Wale siwaamini. Nataka unisuke wewe mwenyewe.”

“Mbona Suzana anajua, tena ananishinda mimi. Umemuogopa bure. Yule ndiye ninayemtegemea sana kusuka watu kwenye saluni yangu.”

“Kwani aliyekusuka wewe ni nani?”

“Ni yeye. Unaonaje, si nimependeza?”

“Kupendeza umependeza, mashallah! Basi itabidi nirudi. Kwani wewe utatoka saa ngapi?”

“Bado, bado nipo kwanza.”

Ghafla Raisa akaziona zile funguo za gari ya Shefa nilizoziweka kwenye kochi.

“Wewe umeniambia Shefa hakuja kwako, mbona hizi funguo za gari lake zipo hapa?” akaniuliza huku akizishika.

Moyo wangu ukapiga kwa kishindo.

Amejuaje kama ni funguo za gari la Shefa!

“Hizo ni funguo za mume wangu,” nikamwambia kwa mkazo.

“Kwani mume wako ana gari?”

“Alikuja nazo yeye, akazisahau hapo hapo.”

Raisa akaanza kuzikagua zile funguo.

“Hizi funguo ni za gari la Shefa, ninazijua. Angalia, zimenadikwa Rav 4. Angalia.”

Raisa akanionesha. Kweli ziliandikwa Rav 4, ambayo ni aina ya gari la Shefa.

“Hebu niambie ukweli kama alikuja kwako jana?”

“Hakuja. Kama angekuja, si ningekwambia shoga. Nikufichie nini?”

“Sasa hizi funguo za gari lake zimefikaje hapa?”

Jinsi Raisa alivyokazana, niliomba Mungu akitoka pale asilione lile gari la Shefa. Nikajiambia, kama ataliona, nijue kuwa sitakuwa na utetezi. Kwa vyovyote vile angerudi haraka na kuniambia gari la Shefa lipo pale na funguo zake ndiyo hizo.

“Hizo funguo si za gari la Shefa. Zilikuja na mume wangu. Alipoondoka akazisahau,” nikamwambia.

“Kinachonishangaza ni kuwa mume wako hana gari. Mwenye gari ni wewe.”

“Sijui mwenyewe alizipata wapi. Lakini magari aina ya Rav 4 si yapo mengi hapa Tanga. Ukiona funguo iliyoandikwa Rav 4 basi ni ya Shefa tu? Shefa mwenyewe hajulikani yuko wapi.”

Nikamalizia kwa kutoa kicheko cha uongo kumzuga.

“Tena nimesikia lori lake limepinduka huko Mabokweni.”

“Mke wake amekuja kuniambia. Na Shefa mwenyewe anatafutwa na polisi.”

“Anatafutwa kwa sababu gani?”

“Mke wake amembiwa lori hilo halina bima na limeshaua. Si umesikia dereva wake amekufa hapo hapo?”

“Nimesikia. Sasa tuseme huyo mwenyewe amekimbia aliposikia anatafutwa na polisi, kwa maana nimesikia hilo lori lilipinduka usiku.”

“Inawezekana alipata habari mapema akaamua akimbie.”

“Sasa kama aliamua kukimbia, angemfahamisha mke wake. Kwa nini anamuacha na wasiwasi? Na huko alikokimbia atakimbia hadi lini?”

Nilikuwa nimeshapata wazo la kumtoa Raisa pale nyumbani. Nilitaka nimtoe kwa gari langu na kumpeleka huko saluni. Lengo langu ni kuwa sikutaka alione gari la Shefa. Kwa kidomodomo chake, kama angeliona, angeleta maneno ambayo sikuyataka.