Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani zinaendelea kupamba moto nchini. Huu ni wakati mwingine ambao ama Watanzania watadanganywa kwa ahadi hewa zisizotekelezeka, au kuambiwa ukweli na wanasiasa wenye dhamira ya kweli.
Kwa uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 30 katika chumba cha habari nikiripoti siasa, safari hii nimeamua kujikita katika kampeni za wagombea urais pekee.
Kupitia makala hizi, nitajaribu kuwasaidia Watanzania wenzangu kutofautisha ahadi zinazotekelezeka na zile za ulaghai, ili mwisho wa siku wapige kura kwa kufanya uamuzi wenye ufahamu.
Hakuna kitu chenye nguvu kuliko imani. Mtu akiamini jambo fulani, imani hiyo humjengea nia na msukumo mkubwa wa kutenda.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa sisi ni masikini na wanyonge na kwa kuamini hivyo, tukajikuta tunaishi maisha ya unyonge na umasikini.
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema hakuna umasikini mbaya kama umasikini wa fikra. Akilitoa mfano Azimio la Arusha, alisema: “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena.”
Hata hivyo, mapinduzi hayo yamekuwa zaidi ya kifikra huku kauli za unyonge zikiendelea kurudiwa, jambo lililotuaminisha kuwa kweli sisi ni masikini. Hadithi hiyo inaendelea hadi leo. Hata ndani ya chama kinachotawala, bado yapo madai kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) ni cha wanyonge, jambo linaloendeleza fikra za unyonge badala ya kuziondoa.
Hivi karibuni nilitazama mahojiano kati ya mtangazaji nguli Tido Mhando na mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz. Nilijiwazia kuwa endapo Rais Samia Suluhu Hassan atamsikiliza Rostam na kumtumia kwa nafasi sahihi serikalini, taifa letu lingeweza kunufaika.
Kwa sababu tatizo kubwa tulilonalo si rasilimali, bali umasikini wa fikra. Tunahitaji kubadilisha mtazamo kutoka kwenye mawazo ya kimasikini kwenda kwenye mawazo ya kitajiri.
Katika muktadha huo, nampongeza mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan. Tofauti na viongozi wengi waliotangulia, ameanza kutumia kile ninachokiita “kauli umba,” yaani kauli chanya zinazojenga fikra za matumaini na kuondoa unyonge.
Hata kama huenda yeye mwenyewe hajitambui kutumia mbinu hiyo, matokeo yake yanaonekana wazi.
Ndani ya ilani ya CCM ya 2025/2030, bado zipo kauli hasi zinazotaja unyonge, lakini hatua ya Samia kuzikataa hadharani ni mwanzo mzuri wa kujenga Tanzania mpya.
Kauli za viongozi wetu kwa muda mrefu zimekuwa zikitufanya tuamini umasikini na unyonge, kumbe kwa hakika Tanzania ni nchi tajiri na Watanzania wana uwezo mkubwa. Ni kauli za kinyonge ndizo zimekuwa zikitufanya tujione duni.
Nimekuwa nikifundisha kupitia makala na mitandao kuhusu dhana ya ‘manifestation’ jinsi kauli chanya zinavyoweza kubadili maisha.
Kauli zinazojenga zinatengeneza hali halisi mpya, wakati kauli za unyonge huendeleza umasikini.
Mfano bora wa kauli umba, ni ule uliotolewa na mgombea wa CCM, Samia alipohutubia maelfu ya wananchi mkoani Iringa.
Alisema: “Kuna maneno wanasema hii serikali si ya wanyonge. Nami nikajibu: siongozi wanyonge, ninaongoza Watanzania.”
Kauli hii ilifuta dhana ya Watanzania kama wanyonge na badala yake ikawapa heshima kama raia kamili wa taifa lao.
Kitendo cha Samia kuikataa dhana ya unyonge ni hatua ya kihistoria. Ni somo kwa wagombea wote wa urais, kutoka vyama vyote 17 vinavyoshiriki uchaguzi huu kuhakikisha wanatoa kauli zinazojenga mshikamano, matumaini na mshikikano wa kitaifa badala ya kauli zinazogawa au kudhoofisha Watanzania.
Methali ya Kiswahili isemayo ‘Penye nia pana njia’ inafafanua vyema nia ya Samia ya kuachana na kauli hasi. Tukidumisha mtazamo huu, taifa letu litaondokana na unyonge na umasikini unaotokana na mitazamo mibaya.
Hapa ndipo chama tawala na upinzani vinapoweza kushirikiana kwa vitendo, kuiga yale yaliyo mazuri kutoka kwa kila upande kwa masilahi ya taifa. Tanzania si mali ya chama fulani, bali ni mali ya Watanzania wote.
Kwa mantiki hiyo, kauli mpya za kujenga ndizo zitakazotufikisha kwenye taifa lenye mshikamano na ustawi.
Nawatakia Watanzania kampeni njema na mwisho wa safari hii, Mungu ataendelea Kuibariki Tanzania.