Dar es Salaam. Viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo watalazimika kugawana kumbi za Mahakama katika kufuatilia mienendo ya kesi mbili tofauti zinazokihusisha chama hicho.
Kesi hizo zimekuwa zikiwakutanisha mahakamani wana-Chadema hao ni kesi ya madai inayokikabili chama hicho kuhusiana na mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama kati ya Bara na Zanzibar na kesi ya jinai inayomkabili mwenyekiti wao, Tundu Lissu.
Kesi hizo zimekuwa zikiwakutanisha mahakamani wana-Chadema hao kwa nyakati tofauti na wakati mwingine katika Mahakama tofauti, lakini leo kesi hizo zinawakutanisha katika Mahakama moja na kwa wakati mmoja.
Leo Jumatano, Septemba 10, 2025, kesi hizozimepangwa kuendelea kusikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, katika hatua tofauti tofauti na mbele ya majaji tofauti.
Katika mazingira hayo, tofauti na nyakati nyingine ambapo wana Chadema hao wote wamekuwa wakikutana kufuatilia kesi moja moja, hivyo leo watalazimika kujigawa katika kesi zote hizo.
Kesi ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga leo imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri dogo la maombi lililofunguliwa na walalamikaji, wakiomba Mahakama iwaamuru walalamikiwa wawapatie nyaraka mbalimbali ambazo wanatajia kuzitumia katika kuthibitisha madai yao.
Awali, kesi hiyo ilikuwa imepangwa Agosti 28, 2025, pamoja na mambo mengine, kwa ajili ya pande zote kuandaa hoja zinazobishaniwa (issues), kutokana na madai yaliyoainishwa kwenye kesi hiyo, ambazo zitaiongoza Mahakama kufikia uamuzi kulingana na ushahidi utakaotolewa na pande zote.
Hata hivyo, siku hiyo wakili wa walalamikaji, Shaban Marijani akishirikiana na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, aliieleza Mahakama kuwa wamefungua shauri jipya la maombi ya nyaraka muhimu kutoka kwa wadaiwa, ambazo wanakusudia kuzitumia katika kesi hiyo kuthibitisha madai yao.
Walalamikaji hao wanaomba wapewe na chama hicho nyaraka saba tofauti tofauti, zikiwemo zinazoonesha mali zinazomilikiwa na chama, za kifedha na za vikao, kwa kipindi cha miaka sita, 2019 mpaka 2024.
Nyaraka hizo ni tamko la mwaka la mali zinazomilikiwa na chama hicho, taarifa za kifedha za chama hicho zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na miktasari ya vikao vya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Nyingine ni miktasari yote ya agenda za vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho, miktasari yote ya agenda za vikao vya Kamati Maalumu ya Zanzibar na miktasari yote ya agenda za vikao vya sekretarieti ya Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema Zanzibar.
Pia taarifa za kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, iliyoko katika Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce Limited).
Hivyo, wakili Marijani aliiomba kesi hiyo ya msingi isimame kwanza kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa shauri hilo la maombi ya nyaraka hizo, kwa kuwa zina athari katika mwenendo wa kesi ya msingi, hoja ambayo iliungwa mkono na mawakili wa walalamikiwa.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa walalamikiwa, Hekima Mwasipu, aliieleza Mahakama kuwa wanakusudia kuwasilisha kiapo kinzani kupinga maombi hayo na wakaomba muda wa siku saba kuwasilisha majibu yao pamoja na kiapo hicho kinzani.
Jaji Mwanga alipanga kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo ya walalamikaji ya nyaraka leo, pamoja na kutaka kesi ya msingi.
Kwa kuwa walalamikaji walishaieleza Mahakama kuwa watawasilisha pingamizi dhidi ya maombi hayo, leo Mahakama itasikiliza kwanza pingamizi la walalamikaji, ambalo kinapaswa kuamuliwa kwanza kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo, kutegemeana na uamuzi wa pingamizi hilo la walalamikaji.
Kulingana na madai yao katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaomba Mahakama hiyo pamoja na mambo mengine itoe amri ya kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika, na iwaamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa akiwa raia wa Tanzania, tarehe hiyo, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Anadaiwa kuwa kwa kuthibitisha nia hiyo ya uasi, alimshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwa maneno aliyoyatamka na kuyaandika.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu, linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde kutoka Mahakama Kuu Bukoba.
Hata hivyo, jana, Lissu aliibuka na pingamizi akipinga Mahakama hiyo kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo, akidai kuwa ni batili kutokana na kasoro za kisheria katika hati ya mashtaka na kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.
Leo, Jamhuri itaendelea na kujibu hoja za Lissu kabla ya Lissu pia kutoa majibu ya kusawazisha hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Jamhuri katika majibu yake.