Mgombea urais Chaumma amnadi mgombea udiwani wa ACT-Wazalendo

Mara. Katika hali isiyotarajiwa na ya kuvutia katika medani ya siasa za upinzani nchini, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amemnadi hadharani mgombea udiwani wa chama cha ACT-Wazalendo, Charles Machemba, katika Kijiji cha Kata ya Ikoma, mkoani Mara.

Hatua hiyo imeibua gumzo katika medani ya siasa, mjadala mpya kuhusu mshikamano wa vyama vya upinzani na uwezekano wa kuunganisha nguvu katika baadhi ya maeneo ili kuleta mabadiliko halisi kwa wananchi.

Mwalimu, licha ya kuwa kwenye kampeni ya kuwania urais kupitia Chaumma mkoani Mara, amesisitiza umuhimu wa kuweka kando tofauti za kiitikadi pale panapohitajika uongozi bora.

“Nipo tayari kumpatia ushirikiano hadi atoboe kuwa diwani hapa,” amesema Mwalimu huku akimwelezea Machemba kama kiongozi anayefaa kupewa nafasi.

Amewaasa wananchi kuachana na masihara na kumchagua mtu bora mwenye uwezo wa kuwatumikia kwa uadilifu na ufanisi.

 “Hatuwezi kuweka tofauti za kiitikadi mbele ya mtu anayeweza kusaidia wananchi. Suala la uongozi halihitaji mzaha, ndiyo maana nasisitiza, acheni masihara na mazoea katika suala la kupiga kura.”

Kwa upande wake, Charles Machemba ameeleza kushangazwa kwake na hatua hiyo, akisema hakutarajia kunadiwa na mgombea kutoka chama tofauti, hasa akiwa ni mgombea wa nafasi ya juu kama urais. Ameitaja kama hatua ya kihistoria na baraka kwake binafsi.

Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akimnadi mgombea udiwani wa ACT-Wazalendo Kata ya Ikoma, Charles Machemba, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.



Katika kata hiyo ambayo Chaumma haijaweka mgombea, Machemba amesisitiza kuwa upinzani una nafasi kubwa ya kushinda, akitoa mfano wa kero zinazowakumba wananchi dhidi ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ikiwemo unyanyasaji unaodaiwa kufanywa dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

“Wananchi wamechoshwa na changamoto hizi. Upinzani una nafasi ya kweli kuchukua nafasi hii, na mimi niko tayari kuwatumikia,” amesema.

Vile vile, hatua hiyo ya vyama vya upinzani kuonesha dalili za kuungana ili kuleta mabadiliko ya kweli katika baadhi ya maeneo imeanza kuwagusa hata wananchi waliokuwa waaminifu kwa sera za uthabiti wa Mwalimu.

Wakizungumza kwa msisitizo, baadhi ya wakazi wamesema mwelekeo huo mpya unaweza kuwa suluhisho la changamoto za maendeleo katika maeneo yao.

“Unajua wananchi siku zote tunahitaji kupata watu wenye dhamira ya kweli katika kutupigania kuhusu mustakabali wa masilahi yetu.

“Mfano, hapa kwetu kata yetu changamoto ni nyingi, lakini diwani aliyekuwepo ni kama alikuwa amejitenga na wananchi wake,” amesema Amos Marwa, mkazi wa eneo hilo.

Marwa ameongeza kuwa licha ya vyama vya siasa kuwa majukwaa muhimu kwa ajili ya kupata uongozi, bado vina upungufu mkubwa katika kushughulikia matatizo ya wananchi.

Amesema kuwa iwapo mfumo ungewaruhusu wagombea huru kwa urahisi zaidi, basi vyama vingi visingeweza hata kuambulia kupata wagombea.

“Katika mambo ya msingi hatuwaoni. Wanajificha, matatizo yanabaki kuwa yetu. Msimu wa uchaguzi ukifika unawakuta wamejaa, wanapita kugonga kila nyumba kutaka kura,” ameeleza Marwa.

Kuunganisha Arusha na Mara

Katika hatua nyingine ya kampeni zake, Mwalimu ameahidi kuunganisha Karatu na Serengeti kwa barabara ya kiwango cha lami ndani ya kipindi cha miaka mitano iwapo atachaguliwa.

Akizungumza mbele ya wananchi wa Serengeti, Mwalimu amesema kuwa licha ya mijadala mizito kuhusu athari za ujenzi wa barabara hiyo kwenye uasili wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na Serengeti, masilahi ya wananchi hayapaswi kupuuzwa.

Kwa sasa, barabara inayounganisha maeneo hayo ni ya vumbi na imekuwa kero kwa watumiaji, huku baadhi ya magari yakikwama msituni, jambo linalodaiwa na Serikali kuwa ni kuepuka kuathiri uasili wa hifadhi hizo muhimu duniani.

“Barabara hii imekuwa na mijadala mingi, lakini mimi nikichaguliwa, nitahakikisha wananchi wa Serengeti na Karatu wanaunganishwa kwa barabara ya lami. Haiwezekani wananchi waendelee kupata shida, wakati magari yangu mwenyewe yalikwama na mengine matatu,” amesema Mwalimu.

Ahadi hiyo ya Mwalimu inakuja baada ya msafara wake kutumia barabara hiyo kutoka Karatu, mkoani Arusha, hadi Mkoa wa Mara, ingawa imeibua mjadala mpya kuhusu namna bora ya kuleta maendeleo bila kuhatarisha mazingira na urithi wa Taifa.

Mwalimu, baada ya kutoka Serengeti, ataelekea Tarime kisha Musoma Mjini, mkoani Mara, kuendelea na kampeni zake za kuuza sera za chama chake kuomba ridhaa kwa wananchi wamchague kushika wadhifa huo.

Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, ambapo Mwalimu na wagombea wa vyama vingine 16 vya siasa wanachuana huku kila chama kimesimamisha wagombea na matumaini ya kuibuka na ushindi.