I&M Bank Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Pesapal Tanzania, kampuni yenye leseni ya kutoa huduma za malipo na suluhisho za kidijitali.
Taarifa iliyotolewa leo Septemba 10,2025 imeeleza ushirikiano huo huu unalenga kupanua upatikanaji wa huduma salama na za uhakika za malipo ya kidijitali kwa biashara nchini Tanzania.
Imesema kupitia ubia huo, I&M Bank Tanzania itawawezesha wateja wake wa biashara kutumia hudumaza Pesapal ikiwemo mashine za Point of Sale (POS), mifumo ya biashara mtandaoni, na malipo ya simu kwa masharti ya upendeleo.
Pia huduma hizo zitawasaidia wafanyabiashara kushughulikia malipo kwa ufanisi, kusimamia miamala kwa urahisi, na kuhudumia wateja wao wa madukani na mtandaoni bila changamoto.
“Mpango huu umeundwa kwa lengo la kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya malipo ya kidijitali
miongoni mwa biashara za Kitanzania, hususan biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na kampuni za ukubwa wa kati.
“Kadri malipo yasiyo ya fedha taslimu yanavyozidi kukua, ubia huu utatoa suluhisho endelevu na rafiki kwa biashara zinazokusudia kupanua huduma na ushindani wao.”
Aidha taarifa hiyo imesema ushirikiano huo pia unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuunga mkono ajenda ya serikali ya ujumuishaji wa kifedha na mageuzi ya kidijitali ya uchumi wa Tanzania. Kupitia huduma hizi, I&M Bank Tanzania na Pesapal zinachangia kuimarisha mfumo wa kifedha wa kisasa na kutoa nafasi kwa biashara kustawi zaidi.
Ubia huo unaiweka I&M Bank Tanzania katika nafasi ya kuendelea kuwa kiongozi wa ubunifu
wa kifedha nchini huku ikihakikisha biashara zinapata nyenzo zinazoongeza ufanisi, usalama,
na urahisi wa huduma za malipo.