Milu Kipimo Apewa Uongozi wa Ukuaji wa Bolt Business Afrika Kusini

Milu Kipimo, raia wa Tanzania, ameteuliwa kuwa Meneja wa Nchi (Country Manager) wa Bolt Business nchini Afrika Kusini (ZA). Kabla ya uteuzi huu, Milu alikuwa Meneja Mkuu wa Bolt kwa Tanzania, Tunisia na Ghana, na sasa anaungana na timu ya Bolt Business Afrika Kusini akiwa na zaidi ya miaka mitano ya uzoefu wa kiuongozi katika biashara, ambapo alishika nyadhifa mbalimbali katika taasisi zinazoongoza sekta ya vyombo vya habari na bidhaa za matumizi ya haraka (FMCG), akiratibu miradi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Katika nafasi yake mpya, Milu Kipimo atakuwa na jukumu la kuendeleza biashara na kukuza timu ya Afrika Kusini, ili kuwasaidia wateja kupata huduma zenye unyumbufu, uzoefu bora wa wateja na usimamizi wa akaunti kupitia Bolt Business kama mbadala wa usafiri wa kibiashara wa jadi.

Juliano Fatio, Mkurugenzi wa Kanda wa Bolt Business, alisema: “Tunafurahi kumpokea Milu katika Bolt Business kuongoza shughuli zetu Afrika Kusini. Uzoefu wake mkubwa alioupata Tanzania, Tunisia na Ghana utatuwezesha kupanua huduma zetu Afrika Kusini na kuleta mtazamo mpya wa kimkakati. Uteuzi huu pia unaonesha dhamira yetu kwa kanda hii, tunapobuni mbinu bora zaidi za kuwatumikia wateja wetu wa kibiashara.”

Kwa upande wake, Milu Kipimo alisema: “Nimeheshimika kujiunga na Bolt Business Afrika Kusini. Natarajia kutumia uzoefu wangu katika nchi za Afrika Mashariki na Kaskazini kuendeleza ukuaji wa kibiashara wenye malengo makubwa sokoni Afrika Kusini, huku nikihakikisha tunawapatia wateja huduma ya ubora wa juu ambayo wanaitarajia kutoka Bolt Business.”

Huduma za Bolt Business Travel ni sehemu ya dhamira ya Bolt ya kuunda miji kwa ajili ya watu, si magari pekee. Tangu kuzinduliwa mwaka 2018, Bolt Business imekuwa ikirahisisha matumizi ya programu ya Bolt kwa mahitaji ya kikazi, ikizisaidia kampuni kupanga usafiri wa wafanyakazi kwa urahisi — kuanzia safari za kila siku hadi matukio ya kikazi — huku ikipunguza urasimu wa makaratasi na malipo ya fidia. Kufikia Desemba 2024, Bolt Business ilipatikana katika zaidi ya masoko 50, ikiwa na zaidi ya kampuni 50,000 zinazotumia huduma hii duniani kote.