DK.SAMIA ATAJA MAFANIKIO LUKUKI UTEKELEZAJI ILANI, AAHIDI MAKUBWA ZAIDI IRAMBA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Singida

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuchanja mbuga katika mikutano ya kampeni kuelekea Uchaguzi mkuu ambapo amehutubia maelfu ya wananchi wa Iramba mkoani Singida.

Akizungumza leo Septemba 10,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Iramba mkoani Singida, Dk. Samia amesema  baada ya kutekeleza Ilani ya uchaguzi kwa miaka mitano iliyopita CCM imejiamini kwa ujasiri kurudi kwa wananchi kuomba ridhaa ya kutekeleza ilani ya uchaguzi 2025 – 2030.

Dk.Samia amesema kwa upande wa utekelezaji Ilani  iliyopita, wagombea ubunge wa Jimbo la Iramba Mashariki na Iramba Magharibi  wameeleza vizuri kwenye afya wamefanya mambo mazuri lakini bado wataendelea kwa sababu wanatambua mahitaji bado yapo.

“Tutaendelea na ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa zahanati lakini kubwa zaidi kusimamia upatikanaji matibabu na dawa kwa wananchi,” alisisitiza.

Dk. Samia alisema serikali inakwenda kuanza majaribio ya bima ya afya kwa wote na bado kuna maradhi ambayo kwa wale wasiokuwa na uwezo serikali itakwenda kugharimia.

“Wale wasiokuwa na uwezo serikali itakwenda kugharamia kwa asilimia 100. Lakini kama mkulima wa choroko, mbaazi na dengu, umeuza na fedha ipo, tunakutaka ununue bima yako ya afya.

Aliongeza: “Lakini wale ambao hawana uwezo kabisa serikali inakwenda kusimamia wananchi wake.”

Kuhusu elimu ,Dk. Samia amesema Serikali  imefanya mengi kwa kujenga vyuo vya ufundi na itaendelea kujenga shule kadri mahitaji yanavyoongezeka.

Akizungumza kuhusu maji katika Wilaya ya Iramba Dk.Samia amesema serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini lakini bado inatambua baadhi ya maeneo kutofikiwa na huduma hiyo.

Amefafanua katika miaka mitano ijayo Serikali itaendelea na miradi ya miji 28, uchimbaji visima lakini kubwa zaidi ni ule mradi mkubwa ambao tukimaliza uchaguzi na mkitupa ridhaa ya kuendesha serikali namkaba Mwigulu azitafute pesa.

“Mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria hadi yapite Singida yaende mpaka Dodoma, mradi ule utakwenda kumaliza shida zote. Sasa fedha tutatoa wapi mimi na yeye tutajua,” alibainisha.

Kwa upande wa Umeme amesema  serikali iliahidi kuweka umeme vijiji vyote ambavyo ahadi hiyo imeikamilisha na kusisitiza kwa sasa huduma hiyo inaunganishwa katika vitongoji.

Pia amesema nishati ya umeme imewafikia hadi wachimbaji ili kuwawezesha kupata urahisi wa uchimbaji na kujiimarisha kiuchumi.”Kwa hiyo tutaendelea kupeleka vijijini umeme kwa wananchi, lakini ndani ya Singida kulikuwa na mradi wa umeme wa upepo.

Ameongeza mradi huo utagharimu Sh.bilioni 80 na tayari wameshafikia pazuri, na kwa sasa wanamtafuta mmbia ili kutekeleza mradi huo wa kuzalisha umeme wa upepo.

“Lengo letu ni kuongeza kiwango cha umeme ili maendeleo yanayokuja yatukute tukiwa na umeme wa kutosha, lakini pia nishati safi inayotokana na maji, upepo, jua, joto ardhi na tuachane na nishati inayotokana na diseli,”amesema Dk.Samia

Pamoja na hayo mgombea Urais,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewaomba wananchi kuipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu ili Serikali ya Chama hicho ikafanye mambo makubwa zaidi kwa wananchi wa Iramba ikiwemo kuendelea kutatua changamoto ya uhaba wa maji na kuifungua Iramba kwa barabara.