WAKAZI wa wilaya ya Kisarawe na maeneo ya jirani wanatarajia kunufaika na huduma za afya bure kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali ya wilaya hiyo.
Madaktari hao ambao wamekuwa wakifanya kazi katika hospitali ya wilaya wataweka kambi ya siku tatu kuanzia Septemba 15 hadi 17 kutoa huduma za kibingwa bure.
Akizungumza ofisini kwake jana Daktari bingwa wa wanawake wa Hospitali hiyo Dk.Hamza Mzige alisema tangu hospitali hiyo kuanzishwa haikuwa na huduma za kibingwa hadi mwaka 2023 walipoletwa madaktari hao.
Amesema kwa muda wote huo hawakuwahi kuweka kambi na kutoa huduma hizo badala yake wamekuwa na siku maalumu ndani ya wiki ambapo wanatoa huduma kwaagonjwa kulingana na uhitaji.
“Tangu hospitali hii ilipoanza hakukuwa na huduma za kibingwa tumesomeshwa na.Serikali na sasa tumerudi kuwahudumia wananchi tuko madaktari bingwa wa watoto, mionzi, masikio, pua na koo “amesema.
Amesema wameamua kufanya kambi hiyi kujitangaza kwa wananchi ambao bado hawana taarifa ya uwepo wao katika Hospitali hiyo ya wilaya ili waweze kufika kutibiwa badala ya kusafiri hadi hospitali ya Amana na Muhimbili.
“Kuna kliniki ambayo tunaifanya kila jumatano na Alhamis wanawake wenye changamoto za uzazi umri wa kuzaa,uvimbe,mimba kutoka na magonjwa mengine yanatibika ndani ya Hospitali ya Wilaya wananchi wafike kupatiwa ufumbuzi”amesema.
Pia Dk Mzige alisema mbali ya kuwa na siku maalumu ya kutoa huduma za kibingwa pia wamekuwa wakifanya kambi kwenye maeneo ya pembezoni ya wilaya hiyo na kukutana na wagonjwa.
Naye Daktari Bingwa wa masikio, pua na koo Dk Andelile Mwaipape aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupatiwa huduma za kibingwa ili wakibainika waweze kupatiwa matibabu mapema.
Dk.Elibarik Munuo ambaye ni Daktari bingwa wa mifupa wa hospitali ya wilaya Kisarawe matatizo ni mengi na wamekuwa wakiwasaidia wagonjwa wengi ikiwemo waliovunjika na wale waliopata bakteria kwenye mifupa ambao wanafanyiwa upasuaji na kupona
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji Charles Sward Luboha alisema wamejipanga kuendesha kambi hiyo kuwasaidia wananchi ambao inaenda sambamba na kuunga juhudi za Rais za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi