Wauza jezi kicheko Simba Day

WAKATI zikisalia saa chache kuanza kwa kilele cha tamasha la Simba Day, asilimia kubwa ya mashabiki wamevalia jezi mpya ya timu hiyo, lakini wafanyabishara wa bidhaa hizo wakichekelea.

Kilele cha wiki ya Simba Day ni siku ambayo hutambulisha wachezaji wapya, benchi la ufundi kitaambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Ali Kiba, Yammi, Mbosso na wengine na ikihitimishwa na mechi ya kirafiki ambayo itacheza na Gor Mahia kutoka Kenya.

Mwanaspoti limeshuhudia asilimia kubwa ya mashabiki waliokuja uwanjani wamevalia jezi mpya ambazo zitatumika msimu huu wa 2025/26.

Mbali na hao wapo ambao wanamiminika kwenye vibanda vya kuuzia jezi hizo wakinunua na kuvaa muda huo.

Asilimia kubwa ni jezi nyekundu zimeonekanika sehemu mbalimbali na buluu kwa baadhi ya watu huku nyeupe ikionekana sehemu chache.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shaaban Ludewa ambaye ni muuzaji wa jezi amesema jezi hizo zinauzwa kwa bei tofauti, nyekundu na buluu ikiuzwa Sh 45,000 na nyeupe Sh 35,000.

Ludewa amefafanua sababu ya kuuza kwa bei tofauti ni kutokana na jezi nyekundu na buluu kuuzika zaidi kuliko nyeupe hivyo amepunguza bei ili nyeupe ipate soko.

Hata hivyo, ameongeza licha ya kupunguza bei bado nyeupe iko chini kwenye mauzo, wengi wao wanainunua nyekundu na nyeupe.

“Hapa tunauza na jezi za misimu iliopita lakini hazihusiki sana wengi wananunua mpya lakini zaidi nyekundu na buluu, nyeupe wengi hawazitaki,” amesema Ludewa na kuongeza;

“Hizi nyeupe ambazo nimepunguza bei wengi wanaume, nimekuja na gari ndogo niliweka lakini nyeupe zimebaki nyingi sana.”

Tamasha la Simba ni la 17 kwa msimu huu tangu lilipoasisiwa mwaka 2009 na litahitimishwa na mechi ya kirafiki ya kimatraifa kati ya timu hiyo na Gor Mahia ya Kenya.