Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema ni haki ya kikatiba kwa wananchi kuhudhuria na kusikiliza mwenendo wa kesi, hivyo hawapaswi kuzuiwa kuingia mahakamani.
Amesema hayo leo nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, ambako inaendelea kusikilizwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
“Mahakama ni ya kiraia na si ya kijeshi. Raia wana haki ya kufika na kusikiliza kesi. Kama ukumbi ni mdogo, basi waingie wale wachache wanaoweza, lakini kwa amani. Kusiwe na vitisho au watu kujitutumua kana kwamba wana nafasi ya kipekee. Shauri linaposikilizwa mbele ya majaji, nguvu ya ushahidi ndilo jambo linalotakiwa kuongoza maamuzi ya mahakama,” alisema Mwabukusi.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuzingatia misingi ya uwazi wa mahakama ili haki ionekane ikitendeka kwa pande zote mbili — mshtaki na mshtakiwa.
Related