Dar es Salaam. Matumizi ya nishati safi ya kupikia yamekuwa ajenda muhimu duniani, hususan katika nchi zinazoendelea ambazo bado zinategemea kuni, mkaa, mafuta ya taa, mabaki ya mimea na vinyesi vya wanyama kwa ajili ya kupikia.
Kutegemea nishati hizo zisizo salama kumechangia kuongezeka kwa matatizo ya kiafya, uharibifu wa mazingira na mzigo wa kiuchumi kwa jamii nyingi.
Tanzania kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imechukua hatua za makusudi kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024/34.
Mkakati huo unalenga kufanikisha upatikanaji wa asilimia 80 ya nishati safi ya kupikia nchini ifikapo mwaka 2034, ukiwa na dhamira ya kupunguza madhara ya kiafya, kulinda mazingira na kuongeza ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa vyanzo vya mpito vilivyoainishwa na mkakati huo ni gesi ya kupikia maarufu LPG (Liquefied Petroleum Gas), ambayo huhifadhiwa kwenye mitungi na hutokana na uchakataji wa mafuta ghafi pamoja na gesi asilia.
LPG ina kiwango cha juu cha propani na buteni, ambacho huchangia kufanya gesi hiyo iwe salama na yenye ufanisi katika matumizi ya nyumbani na taasisi mbalimbali.
Hata hivyo, Tanzania bado inalazimika kuagiza gesi hiyo kutoka nje ya nchi kutokana na ukweli kwamba haina kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi. Gesi asilia iliyogunduliwa nchini haina kiwango cha kutosha cha propani na buteni kinachoweza kuzalisha LPG kwa wingi.
Ripoti ya Utendaji ya Sekta ya Mafuta ya mwaka 2023/24 iliyotolewa na Ewura inaonesha ongezeko kubwa la uingizaji wa LPG nchini.
Katika mwaka huo wa fedha, tani za ujazo 403,638 ziliingizwa kulinganishwa na tani 293,167 zilizoingizwa mwaka 2022/23. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 38.
Takwimu hizo zinaashiria mwamko mkubwa miongoni mwa Watanzania kuachana na matumizi ya kuni, mkaa na mafuta ya taa, badala yake kukumbatia gesi kama nishati safi na ya kisasa ya kupikia.
Masharti ya kuhakikisha usalama
Pamoja na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya LPG, Ewura imeweka kipaumbele katika kuhakikisha usalama wa wananchi.
Hii inahusisha kutoa elimu ya usalama kwa watumiaji na wafanyabiashara, kufuatilia utekelezaji wa kanuni na miongozo ya usalama pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miundombinu ya uhifadhi na usambazaji wa gesi.
Hatua hizo zinachangia kulinda maisha ya watu na mali, sambamba na kujenga imani ya jamii katika kutumia LPG kama chaguo salama na la kuaminika.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Ewura imeweka masharti maalumu yanayopaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha usalama na uadilifu katika biashara ya LPG.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuwa na leseni sahihi kutoka mamlaka husika na cheti cha ukaguzi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Aidha, muuzaji wa LPG anapaswa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na awe na uelewa wa namna ya kuvitumia huku akiwajulisha wateja wake hatua za dharura wanazopaswa kuchukua endapo ajali itatokea.
Masharti mengine ni kutumia mizani iliyothibitishwa na Wakala wa Vipimo (WMA), kuhakikisha mitungi inapimwa na kukaguliwa kabla ya kuuzwa na kuizuia kuhifadhiwa kwenye maeneo yenye vyanzo vya moto.
Pia, ni marufuku kuuza mitungi iliyochakachuliwa au yenye ujazo pungufu, jambo linalosaidia kulinda haki na usalama wa watumiaji.
Kwa watumiaji, Ewura imetoa mwongozo wa usalama unaolenga kupunguza ajali na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.
Kwanza, wananchi wanashauriwa kununua mitungi kutoka kwa mawakala wenye mizani iliyohakikiwa na WMA na kuhakikisha mitungi ina mihuri ya usalama.
Wakati wa usafirishaji, mitungi inatakiwa kusafirishwa ikiwa wima na kuachwa kwa angalau dakika 20 kabla ya kutumika.
Aidha, ili kubaini iwapo mtungi unavuja, mtumiaji anatakiwa kutumia povu la sabuni kwenye sehemu ya valvu na iwapo povu litapungua au kuchemka, hiyo ni ishara ya uvujaji.
Katika tukio la uvujaji wa gesi bila kuwaka moto, mtungi unatakiwa kutolewa nje na kuachwa sehemu yenye hewa ya kutosha.
Endapo gesi inavuja kwa kiwango kinachoweza kudhibitiwa, mtumiaji anaweza kuizuia, lakini kama haiwezekani mtungi uachwe uvuje hadi gesi iishe huku hatua za usalama zikiendelea kuchukuliwa.
Vilevile, mtungi unapaswa kuhifadhiwa mbali na joto kali au vyanzo vya moto, na iwapo utatokea moto mdogo unaweza kuzimwa kwa kutumia vifaa vya kuzimia moto vilivyopo.
Kwa moto mkubwa, wananchi wanahimizwa kuwasiliana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kupiga namba 114.
Ni muhimu pia kufahamu kuwa hata mitungi mitupu ni hatarishi, hivyo tahadhari zote za kiusalama zinapaswa kuzingatiwa.
Zaidi ya hayo, iwapo mtu atahisi harufu ya gesi ndani ya nyumba, hatua ya kwanza ni kufungua madirisha na milango mara moja ili kuruhusu hewa kuingia.
Wakati huohuo, ni marufuku kuwasha taa, vifaa vya umeme au moto wowote kwa sababu vitachochea hatari ya mlipuko.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile, anasisitiza kwamba mamlaka inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha utoaji wa leseni unafanyika kwa haraka na kwa uwazi.
Aidha, Ewura inafuatilia upatikanaji wa gesi sokoni, kuhamasisha usambazaji wake hususani katika maeneo ya vijijini na kuchunguza mwenendo wa bei ili kuhakikisha LPG inabaki kuwa nafuu na kupatikana kwa kila Mtanzania.
Dk Andilile anasema licha ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa gesi, usalama wa matumizi unabaki kuwa kipaumbele kikuu.
Kwa muktadha huo, Ewura inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kusimamia kwa karibu kanuni za usalama zinazohusu wafanyabiashara na watumiaji.
Hii inalenga kuhakikisha kwamba nishati safi ya kupikia inatumika kwa ufanisi bila kuhatarisha maisha, mali na mazingira.
Hatua hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Taifa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanapata nishati safi na salama ya kupikia, jambo litakalosaidia kulinda afya za wananchi, kupunguza ukataji miti hovyo na kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.