TAYARI kumeanza kuchangamka katika Uuwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam ambako Simba ina jambo lake leo kwenye kilele cha Tamasha la Simba Day ikiwa ni sehemu ya kusheherekea miaka 89 ya klabu hiyo.
Achana na mechi za awali ambazo zimechezwa, burudani zimeanza kuchukua nafasi yake hasa kuanzia saa 10:00 jioni.
Ilianza kupigwa ngoma moja baada ya nyingine zenye vaibu huku wanenguaji wakionyesha uwezo wa kuamsha mashabiki muda mchache kabla ya washeheshaji, Meena Ally na Adam Mchomvu kupanda jukwaani.
Baada ya hapo ndipo ulipopigwa wimbo wa ‘Hakuna Mungu kama wewe’ na zaidi ya mashabiki 50,000 ambao wamefurika uwanjani wakanyanyuka kwenye viti na kuimba sambamba na Kwaya ya Uinjilisti ya Kijitonyama.
Mara baada ya tukio hilo ndipo Mchomvu na Meena wakaendelea na ratiba ya kukaribisha wasanii mmoja baada ya mwingine. Miongoni mwa wasanii wa kwanza kushusha burudani ni mwamba wa Kaskazini, Joh Makini.
Burudani hizo zitafuatiwa na mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Simba dhidi ya Gor Mahia ya Kenya baada ya utambulisho wa wachezaji ambao watawatumikia wana Msimbazi msimu ujao wa mashindano.