Mahakama yazuia Trump kumfukuza kazi Gavana wa Benki Kuu

Washington. Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Shirikisho, Jia Cobb, amezuia kwa muda utekelezaji wa uamuzi wa Rais Trump wa kumfukuza kazi Gavana wa Benki Kuu, Lisa Cook.

Cook, ambaye ni mjumbe wa bodi inayowajibika kuweka viwango vya riba nchini Marekani, alifukuzwa kazi na Trump kwa madai kwamba alitoa taarifa za uongo katika maombi ya mkopo wa nyumba mwaka 2021, kabla ya kuwa Gavana wa Benki Kuu.

Hata hivyo, uamuzi wa Jaji Cobb, alioutoa leo, Septemba 10, 2025 umeelezwa kama ushindi kwa Benki Kuu katika kesi ya kihistoria dhidi ya Ikulu ya White House kuhusu uhuru wa taasisi hiyo ya fedha.

Mwezi uliopita, Cook aligoma kutekeleza uamuzi wa Trump wa kumfukuza kazi, akidai hana mamlaka hayo.

Jaji Cobb, katika uamuzi wake, amesema uamuzi wa Trump kumwondoa Cook ofisini ulikiuka sheria inayounda Benki Kuu.

“Kulingana na sheria hiyo, iliyoundwa kulinda Benki Kuu dhidi ya kuingiliwa kisiasa, magavana wanaweza kuondolewa tu kwa ’sababu ya msingi’,” amebainisha Jaji Cobb, na kuongeza kuwa:

“Ili kufanikisha kufukuzwa, sababu hiyo lazima iwe imejikita katika mwenendo mbaya wakati akiwa kazini.”

Jaji Cobb pia ameamua kuwa Trump huenda alivunja haki ya Cook ya kufanyiwa mchakato wa haki, na kwamba kumfuta kazi kungeleta ‘madhara yasiyorekebishika’ kwa gavana huyo.

“Uamuzi huu unatambua na kuthibitisha umuhimu wa kulinda uhuru wa Benki Kuu dhidi ya kuingiliwa kisiasa kinyume cha sheria,” amesema wakili wa Cook, Abbe Lowell, katika taarifa.

Pia ameongeza kuwa: “Kumruhusu Rais amwondoe Gavana Cook kinyume cha sheria kwa madai yasiyothibitishwa na yasiyoeleweka vyema kunaweza kuhatarisha uthabiti wa mfumo wetu wa kifedha na kudhoofisha utawala wa sheria.”

Hata hivyo, Jaji Cobb kwenye uamuzi wake huo amesema: “Rais Trump hajabainisha jambo lolote linalohusiana na mwenendo au utendaji wa kazi wa Cook kama mjumbe wa bodi ambalo linaonesha kwamba anadhuru bodi au masilahi ya umma kwa kutotekeleza majukumu yake kwa uaminifu au kwa ufanisi.

“Sababu ya msingi haikusudiwi kumwondoa mtu kwa tabia au vitendo vilivyotokea kabla hajaanza kazi.”

Kutokana na uamuzi huo, msemaji wa White House amesema: “Uamuzi huu si wa mwisho katika suala hili, na utawala wa Trump utaendelea kufanya kazi ya kurejesha uwajibikaji na imani kwa Benki Kuu.

“Rais Trump alimwondoa Lisa Cook kihalali kwa sababu ya madai ya kuaminika ya udanganyifu wa mikopo ya nyumba kutoka kwa nafasi yake nyeti ya kusimamia taasisi za kifedha katika bodi ya magavana ya Hifadhi ya Shirikisho.”

Kesi hiyo ambayo huenda ikaishia katika Mahakama Kuu ya Marekani, inaonekana kuwa muhimu kwa uwezo wa Benki Kuu kuweka viwango vya riba bila kuathiriwa kisiasa.

Rais Trump amekuwa akiikosoa mara kwa mara Benki Kuu, hasa mwenyekiti wake Jerome Powell, kwa kutopunguza viwango vya riba huku benki kuu za Ulaya na Uingereza zikipunguza gharama za mikopo.

Wakili wa Cook, Abbe David Lowell, amesema: “Uamuzi huu unatambua na kuthibitisha umuhimu wa kulinda uhuru wa Benki Kuu dhidi ya kuingiliwa kisiasa kinyume cha sheria. Gavana Cook ataendelea kutekeleza majukumu aliyokula kiapo kuyatekeleza kama gavana aliyeidhinishwa na Seneti.”

Cook alimshtaki Trump kutokana na jaribio lake la kumfuta kazi, hatua iliyosababisha mgogoro wa kisheria wenye athari kubwa kwa uhuru wa Benki Kuu ya Marekani.

Trump na mkurugenzi wa Mamlaka ya Nyumba na Fedha ya Shirikisho, William Pulte, wamedai kuwa Cook alitoa maelezo yasiyo sahihi kuhusu mali tatu tofauti katika maombi ya mikopo ya nyumba, jambo lililomuwezesha kupata viwango vya chini vya riba na mikopo ya kodi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais kujaribu kumfukuza gavana wa Benki Kuu, na sheria hiyo haijawahi kujaribiwa mahakamani.

Benki Kuu inatarajiwa kukutana wiki ijayo kutangaza upunguzaji wake wa kwanza wa viwango vya riba tangu Septemba 2024.

Elidaima Mangela kwa msaada wa Mashirika