TANZANIA YAORODHESHWA KATIKA NCHI ZINAZOTAZAMIWA KUFUZU KUTOKA NCHI MASIKINI

Na. Peter Haule na Joseph Mahumi, WF, Dodoma

Tanzania imeorodheshwa na Kamati ya Sera za Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, kuwa miongoni mwa nchi zinazotazamiwa kufuzu kutoka katika kundi la nchi masikini (Least Developed Countries) kwenda nchi inayoendelea.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati wa Mkutano wa Awali wa tathmini ya nchi kutoka nchi maskini kwenda nchi inayoendelea inayofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

Dkt. Mwamba alisema hatua hiyo imetokana na Tanzania kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kupitia uthabiti wa Sera za uchumi zilizosababisha kukua kwa uchumi kwa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2000 na 2024.

“Pato la mtu kwa mwaka limeongezeka kutoka dola za Marekani 453 mwaka 2000 hadi dola 1,277 kwa mwaka 2023, kiwango cha umasikini uliokithiri kimepungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2024 kutokana na utekelezaji makini wa sera za fedha na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi”, alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki kwenye tarakimu moja hali iliyoimarisha uthabiti wa uchumi na kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na gharama za maisha.

Alisema kuwa kumekuwa na uwekezaji wa kimkakati hususani katika miundombinu ya nishati kupitia utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere Hydropower ambao ni mradi mkubwa wa kitaifa wa ujenzi na uzalishaji wa umeme.

Alisema kuwa upo mradi wa usafiri wa abiria na mizigo kati ya Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma kupitia Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) na pia miradi ya maboresho katika sekta ya elimu na huduma za afya.

Vilevile alisema kuwa maboresho katika elimu na huduma za afya pamoja na mkazo katika viwanda na ajira yamechangia katika kufikia vigezo vinavyowezesha nchi kuondolewa kwenye kundi la nchi maskini.

Aidha, Dkt. Mwamba ameishukuru Timu ya wataalamu wa Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) ambalo limeanza hatua za awali za tathmini ya nchi kutoka nchi maskini kwenda nchi inayoendelea na kuahidi Serikali kutoa ushirikiano thabiti ili kufanikisha zoezi hilo.

Aidha, Dkt. Mwamba alisema kuwa Serikali ina imani na ziara hiyo ya wataalamu wa tathmini kwa kuwa pia itatoa mchango katika maendeleo ya nchi na kusaidia juhudi za Serikali za koboresha sera zitakazoifanya Tanzania kuwa imara zaidi, yenye usawa na mafanikio kwa wote.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mhe. Shigeki Komatsubara, alisema kuwa Umoja wa Mataifa upo tayari kuisaidia Tanzania kufanikisha kwa urahisi kuwa katika uchumi wa kati.

Amesema hatua ya sasa ya tathmini ni sehemu ya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Washirika wa Maendeleo na Tanzania.

Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na yeye kama mratibu wa zoezi hilo ni shirikishi litakalosikiliza sauti za watanzania wa rika zote.

Alisema maendeleo yanayotarajiwa yatafikiwa iwapo yatawashirikisha watu wote waliolengwa katika mikakati ya maendeleo.

Mkutano huo ulishirikisha wadau wa taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, Asasi zisizo za Serikali na za Kiraia, Washirika wa Maendeleo Tanzania Bara na Zanzibar ambayo yatatumika katika kuandaa tathmini hiyo kwa njia ya mahojiano.

Zoezi la tathmini lina lengo la kusaidia nchi kujiimarisha kimuundo, kijamii na kiuchumi pamoja na kuainisha changamoto na fursa katika kipindi cha maandalizi ya kuhitimu na baada ya kuhitimu kutoka kwenye kundi la nchi masikini.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Awali wa Tathmini ya nchi kutoka katika kundi la nchi Maskini kwenda nchi inayoendelea inayofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), uliofanyika katika ukumbi wa Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuwa Serikali ina imani na ziara hiyo ya wataalamu wa tathmini kwa kuwa pia zoezi hilo litatoa mchango katika maendeleo ya nchi na kusaidia katika kuunda sera zitakazoifanya Tanzania kuwa imara zaidi, yenye usawa na mafanikio kwa wote.