Historia mpya, washtakiwa 30 wakiri makosa ya ugaidi

Dar es Salaam. Linaweza kuwa moja ya matukio nadra kutokea katika usikilizwaji wa kesi, baada ya washtakiwa wote 30 kukiri makosa kadhaa ya ugaidi na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita jela, baada ya kusota gerezani kwa miaka 10.

Uamuzi wa washtakiwa kukiri makosa ya ugaidi unaingia katika matukio yaliyovunja rekodi katika haki jinai, hasa ikizingatiwa kuwa kukiri kwao kumekuja wakati shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri akijiandaa kutoa ushahidi.

Hukumu hiyo imetolewa Septemba 9, 2025 na Jaji Gabriel Malata wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, aliyewaondolea miaka 10 waliyokaa gerezani katika kifungo cha miaka 16 ambacho ndicho walikistahili.

Kosa la kwanza la kula njama ya kutenda matendo ya kigaidi na la 14 la kushiriki mikutano ya kupanga ugaidi yaliwakabili washtakiwa wote 30, lakini baadhi yao pia walikabiliwa na makosa mengine ya ugaidi.

Makosa hayo ni kuanzia la pili hadi la 13 ambayo yanahusisha kuhamasisha vitendo vya ugaidi, kuandaa mikutano ya kusaidia kufanyika mikutano ya kuandaa matendo ya ugaidi na kutoa mali ili zitumike kutekeleza vitendo vya ugaidi.

Mbali na makosa hayo, walikabiliwa na mengine ya kutafuta watu wa kutekeleza ugaidi na kukutwa na vitu kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi, ambavyo ni pamoja na bunduki ya kivita aina ya Avtomat Kalashnikova (AK-47).

Pia, baadhi ya washtakiwa walipatikana na risasi, visu, mapanga, fulana mali ya Jeshi la Polisi Tanzania, suruali moja mali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), bomu lililotengenezwa kienyeji na malighafi za milipuko.

Upande wa Jamhuri uliokuwa na jopo la mawakili wa Serikali wakuu, Valence Mayenga, Esther Martin na Geofrey Mlagala, wakishirikiana na mawakili wengine wa Serikali, ulidai makosa hayo yalitendeka tarehe tofauti mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Jaji Malata, kesi hiyo imehusisha mawakili 45 wa Jamhuri na utetezi, na akatumia hukumu hiyo kuwapongeza kwa weledi wao na namna walivyoisaidia Mahakama kufikia hitimisho la kesi hiyo.

Washtakiwa kwa pamoja walishtakiwa kwa kuajiri, kukodi watu na kutekeleza misheni ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kumiliki silaha kwa lengo la kutishia umma na kuanzisha utawala wa Kiislamu Tanzania.

Washtakiwa ni Jaffar Hassan, Sadick Shaban, Ibrahim Abdallah, Said Mtulya, Ally Ngingo, Said Nkuri, Juma Ally, Shomary Ngwabi, Issa Hassan, Nurdin Mhagama, Hamad Juma, Ahamad Ndulele, Hamis Seleman na Hamis Hussein.

Wengine ni Ally Ngachoka, Abdallah Lupindo, Abdubillah Ndebalema, Shaibu Mkungu, Seif Mbwate, Hassan Abdallah, Abdurashid Sadiki, Paulo Mgita, Abdallah Mohamed, Abbas Mkanda, Nassoro Hemed, Rajabu Chijeja, Mohamed Omari, Said Mandanda, Shafii Mputeni na Twalha Mwaluka.

Ilivyokuwa wakakiri makosa

Agosti 17, 2023 washtakiwa walifikishwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH) wa kesi dhidi yao. Walisomewa mashtaka 14 yanayohusu ugaidi na wote walikana mashtaka.

Kukana kwao mashtaka kuliufanya upande wa Jamhuri kuita mashahidi kuthibitisha mashtaka, huku washtakiwa wakipewa msaada wa kutetewa na jopo la mawakili 30 kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) walioteuliwa na Mahakama.

Septemba mosi, 2025 washtakiwa walifikishwa mahakamani kuendelea na usikilizwaji wa kesi. Jopo la mawakili wa utetezi liliieleza Mahakama kuwa wateja wao wanaomba wakumbushwe mashtaka dhidi yao.

Upande wa Jamhuri ulisomea mashtaka kwa lugha ya Kiswahili ambayo washtakiwa waliielewa. Awali walikana kufanya makosa hayo, lakini baadaye walibadilisha msimamo wao na kukiri kuwa walitenda makosa hayo.

Mahakama ikawaalika upande wa Jamhuri kusoma maelezo ya namna makosa yanayowakabili yalivyotendeka. Baada ya kusomewa, mshtakiwa mmoja baada ya mwingine alikiri kuwa maelezo hayo ni sahihi na ndivyo ilivyokuwa.

Mahakama ikawatia hatiani washtakiwa kila mmoja kwa namna alivyoshtakiwa. Jukumu lililobaki likawa ni kuwasomea adhabu. Lakini kabla ya kufanya hivyo, Mahakama iliwapa fursa ya kuwasilisha maombolezo (mitigation) ya kupunguziwa adhabu.

Kupitia mawakili wao, washtakiwa walieleza kuwa walikamatwa mwaka 2014 na kwamba wameshakaa mahabusu kwa miaka 11, na wamekiri makosa yao pasipo kuisumbua Mahakama, pia wanajutia kile walichofanya.

Mbali na hilo, walieleza wao ni wakosaji wa mara ya kwanza na hilo lilithibitishwa na Jamhuri. Vilevile, asilimia 95 ya washtakiwa wana umri chini ya miaka 40, hivyo ni vijana wanaohitajika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya nchi.

Walisema wana familia, wenza na watoto ambao waliwaacha miaka 10 iliyopita na wanahitaji msaada wao kwa ajili ya mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi na malazi.

Mbali na hayo, wana wazazi wazee wanaohitaji msaada wao. Pia walitelekeza familia zao kutokana na kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu, baadhi yao wanakabiliwa na maradhi yanayohitaji matibabu nje ya gereza na wanaahidi kuwa raia wema.

Katika hukumu hiyo, Jaji Malata alichambua sheria inayosimamia makosa ya ugaidi na kufafanua namna adhabu kwa makosa hayo ni kifungo kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 20 gerezani, lakini akazingatia maombolezo waliyoyatoa.

“Ni wazi Mahakama hii haiwezi kutoa kifungo chini ya miaka 15 wala kinachozidi miaka 20. Kutokana na msimamo huo, Mahakama inawahukumu kutumikia kifungo cha miaka 16 jela kwa kila kosa na vitatumikiwa pamoja,” amesema Jaji na kuongeza:

“Baada ya kuwahukumu adhabu hiyo, Mahakama sasa itatizama sababu zile za maombolezo ya kuonewa huruma zikigusa muda wa miaka 10 waliokaa gerezani wakisubiri kukamilishwa kwa kesi yao.”

Jaji Malata amesema hakuna ubishi kuwa washtakiwa wamekaa gerezani tangu mwaka 2015, ambayo ni muda wa miaka 10 unaopaswa kuzingatiwa katika kifungo cha miaka 16 alichowahukumu kutokana na makosa yao.

Baada ya kuzingatia muda huo, Jaji amesema Mahakama inachukulia muda huo kama sehemu ya adhabu ambayo wameshaitumikia, hivyo utapunguzwa kutoka katika adhabu ile ya miaka 16 na kubakia na miaka sita gerezani.