Taifa yaimba na Mbosso | Mwanaspoti

Ni burudani tu ndani ya Uwanja wa Mkapa katika Simba Day, ambapo mashabiki wa Simba wameimba pamoja na msanii Mbosso.

Mbosso ambaye ameanza kwa kuimba wimbo wake mpya wa Selemani kabla ya kuimba vigongo vyake kadhaa amewateka zaidi 
mashabiki kwa kuimba nao ‘live’ wimbo wake wa ‘Haijakaa sawa’ ambao aliutoa wakati yupo chini ya lebo ya Wasafi.

Wakati burudani hiyo inaendelea kwa nyakati tofauti mashabiki wamesitisha zoezi hilo ili kushangilia baadhi ya viongozi wao waliokuwa wanaonyeshwa kwenye skrini za uwanjani hapo.

Viongozi ambao walionyeshwa ni pamoja na Babra Gonzalenz ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi. Mwanamama huyo aliwahi kuwa ofisa mtendaji mkuu wa klabu huyo miaka ya karibuni ambapo aliiwezesha Simba kutamba ndani na nje ya nchi.

Vilevile, mashabiki hao wamesitisha kwa muda kuimba baada ya kuonyeshwa mwekezaji wao Mohamed Dewji ambaye kwa sasa ni rais wa heshima.

Awali, Mbosso alianza kwa kuimba huku nyimbo zake zikichezwa (play back) kabla ya kuimba ‘live’. Mara kadhaa alipojaribu kuwaambia mashabiki kuwa inatosha na kuwashukuru ikiwa ni ishara ya kuwaaga, uwanja ulisikika ukipiga kelele kupinga.