Dar es Salaam. Mjumbe Maalumu wa Biashara wa Uingereza kwa Afrika Mashariki, Kate Asamor, ameipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua kuboresha mazingira ya uwekezaji, huku akisisitiza dhamira ya Uingereza kuendelea kushirikiana kwa karibu katika miradi ya kimkakati.
Asamor ametoa kauli hiyo leo, Septemba 10, 2025 walipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, katika Jumba la Commons, jijini London.
Amesema Uingereza iko tayari kusaidia upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo.
“Pia, tuko tayari kuimarisha miradi ya miundombinu ya Zanzibar na kusaidia miradi ya kijani na kidijitali,” amesema Asamor.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza kupitia miradi inayoendelea na mipango mipya inayohusisha nishati, madini, uchumi wa buluu, fedha za kijani, ubunifu wa kidijitali na kilimo cha mazao ya biashara.
Kwa upande wake, Waziri Kombo amesema dhamira ya Serikali ni kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuhakikisha miradi inayoungwa mkono na taasisi za kifedha za Uingereza, ikiwemo UK Export Finance (UKEF) na British International Investment (BII), inatekelezwa kwa ufanisi.
“Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria na Uingereza na inatambua mchango mkubwa wa miradi ya uwekezaji katika kuongeza ajira, kukuza biashara ya kikanda na kimataifa, na kuendeleza sekta za kipaumbele kama madini muhimu, nishati safi na uchumi wa buluu,” amesema.
Mbali na biashara, mazungumzo hayo pia yaligusia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, na Waziri Kombo amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi huo unasimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hatua ambayo itaongeza uwazi na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Pande zote mbili zilithibitisha kuendeleza uratibu wa karibu kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) na kukubaliana kuanzisha timu ya ufuatiliaji ya pamoja itakayokuwa na mapitio ya robo mwaka ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa makubaliano yaliyofikiwa.