Moshi. Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Stephen Ngasa, ameahidi akichaguliwa kuwa mbunge, ataelekeza asilimia 40 ya mshahara wake kununua chakula kwa ajili ya wanafunzi yatima na wale wanaotoka katika mazingira magumu kwenye shule za msingi na sekondari.
Mbali na mchango huo wa binafsi, Ngasa pia ameahidi kutumia fedha za mfuko wa jimbo kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu na wanafunzi.
Aidha, ameeleza nia yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuchochea ukuaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.
Ngasa ametoa ahadi hizo wakati akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, uliofanyika katika viwanja vya Manyema, Manispaa ya Moshi, ambapo amesisitiza kuwa dhamira yake kuu ni kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo kwa vitendo na uwazi.
“Nikiwa mbunge, asilimia 40 ya mshahara wangu nitaitumia kununua chakula kwa ajili ya wanafunzi yatima na wale wa mazingira magumu, wanaosoma shule za msingi na sekondari.
“Pia, nitarudisha maeneo yote ya wazi ya umma yaliyoporwa kinyume cha taratibu na kuongeza mapato ya halmashauri kwa kutumia vizuri maeneo ya uwekezaji kama Bustani ya Uhuru Park, ambayo kwa sasa haijatumika ipasavyo,” amesema Ngasa.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo kupitia ACT-Wazalendo, Mohamed Baraka, amesema chama hicho kimejipanga vizuri kuhakikisha kinapata ushindi ili kuleta mabadiliko ya kweli na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Edgar Mkosamali, amewaomba wananchi wa Moshi Mjini kumchagua Ngasa Oktoba 29, 2025uu, ili akalete mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo.
“Moshi ni watu ambao huwa mnataka mabadiliko, sasa tunaomba mumuunge mkono mgombea wetu Stephen Ngasa na kumchagua awe mbunge, kwani kipindi cha nyuma aliwahi kuwa diwani kwa miaka 10 na Moshi anaijua vizuri na changamoto zake,” amesema Mkosamali.