ACT-Wazalendo waita nyomi hukumu ya kesi ya Mpina kesho

Dodoma. Chama cha ACT-Wazalendo kimeita wanachama, wadau na wale wanaotajwa kuwa wapenzi wa demokrasia kujitokeza kwa wingi kesho katika Mahakama Kuu Masijala Kuu Dodoma ili kusikiliza hukumu ya mtiania wao wa urais, Luhaga Mpina.

Kaimu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande, amewaambia waandishi wa habari leo, Jumatano, Septemba 10, 2025, kuwa wanatarajia kuwa na umati mkubwa wa watu.

ACT-Wazalendo, kupitia bodi ya wadhamini na mtiania wa kiti cha urais kwa chama hicho, Mpina, wameishtaki Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakipinga kuzuiwa kupokea fomu za kuwania nafasi hiyo.

Leo Maharagande amesema ACT-Wazalendo hakiwezi kuingilia mchakato mzima wa majaji katika hukumu hiyo, bali wanaomba wapenda haki wajitokeze kwa wingi kuona kinachokwenda kutokea.

“Sisi hatujui mpaka sasa nini kitaamuliwa, isipokuwa tunawaita wanachama na wapenzi wa chama chetu na mgombea kwamba waje Dodoma kusikiliza nini kinakwenda kutokea kesho, Septemba 11, 2025, kuhusu hukumu hiyo,” amesema kaimu katibu mkuu huyo.

Jopo la majaji watatu Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza juzi waliahirisha kesi hiyo baada ya kusikiliza pande zote mbili za mawakili na kuipanga hukumu kesho.

Akizungumza kuhusu kuchelewa kuanza kampeni iwapo watashinda, amesema wanajua na kwamba mtiania wao yuko tayari kushindana hata kwa siku hizo.

Amesisitiza kuwa siku ya kesho wanaitazama kama siku ya demokrasia na haki, ambayo inabeba hatima ya ACT-Wazalendo na Watanzania kwa ujumla, hivyo wale watakaoshindwa kufika Dodoma wameshaombwa kuwa tayari kufuatilia hukumu kupitia mtandao kwa kiunganishi kitakachotumwa mapema.