Dar es Salaam. Ili kuongeza mchango wa uchumi wa buluu katika pato la Taifa, Umoja wa Ulaya umetoa zaidi ya Sh1.08 trilioni kwa benki za biashara nchini ili zikopeshwe kwa makundi yaliyopo katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Fedha hizo, zilizotolewa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), tayari zinatolewa kupitia benki za CRDB, NMB na KCB, huku mazungumzo na benki nyingine yakiendelea. Mpaka sasa zaidi ya biashara ndogo, za kati na vyama 11,000 vimenufaika.
Hayo yamebainishwa leo, Septemba 10, 2025, na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Abdalah Hassan Mitawi, katika mkutano wa kitaifa wa wadau wa uchumi wa buluu 2025 ulio na kaulimbiu ‘Bahari yetu, fursa yetu. Wajibu wetu kuanzia 2021 hadi 2025’.
Mitawi amesema fedha hizo zimeanza kusambazwa katika benki zilizokuwa tayari ili zikopeshe vikundi vya wafanyabiashara au taasisi zinazofanya shughuli za uchumi wa buluu kwa riba ndogo.

“Utaratibu huu umekuwa ukifanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Fedha na Umoja wa Ulaya… umesaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa taasisi za nchi na hata kimataifa,” amesema.
Amesema Taifa linapoelekea kuwa nchi ya kipato cha kati, uchumi wa buluu unabaki kuwa chachu muhimu ya maendeleo kutokana na fursa zilizomo ndani yake ambazo bado hazijatumika, hasa kwa vijana, wanawake na sekta binafsi.
Ofisa Mipango wa Kitengo cha Rasilimali Asilia kutoka EU, Daniel Gonzalez, amesema mbali na fedha zilizotolewa, pia Umoja wa Ulaya umezindua mradi wa euro milioni 15 (Sh43.8 bilioni) unaolenga kuimarisha miundombinu ya uchumi wa buluu kwa kusaidia sekta muhimu kwa ajili ya utengenezaji wa ajira, usalama wa chakula, utalii, biashara na tabianchi.
Amesema ushirikiano huo wa kimkakati na Tanzania umejengwa juu ya misingi ya pamoja ya ukuaji wa uchumi jumuishi, uendelevu wa mazingira na ushirikiano wa kikanda.
“Umoja wa Ulaya ni mshirika muhimu katika biashara ya baharini, uvuvi, utalii na maendeleo ya ukanda wa pwani, kwani inasaidia kutekeleza kwa vitendo maono ya Tanzania kuhusu uchumi wa buluu,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, amesema uwepo wa kongamano hilo unatoa nafasi ya kutambua mchango wa uchumi wa buluu katika pato la Taifa kwa kuangalia fursa zilizopo na changamoto zilizopo ili zitatuliwe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi, Shomari Shomari, amesema kuwa usafiri ni moja ya viunganishi muhimu katika kujenga uchumi wa buluu, hususan bahari.