Neema arejea nchini na ubingwa wa Perm Marathon

Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Neema Msuadi amerejea nchini akitokea Russia alikokwenda kushiriki mbio za Perm Marathon.

Mbio hizo zilifanyika Oktoba, mwaka huu, jijini Perm ambako Neema alimaliza wa kwanza kwa muda wa saa 2:38:15 na kuwa Mtanzania wa pili kuongoza mwaka huu baada ya Gabriel Geay kufanya hivyo mwezi Februari akishinda Daegu Marathon za Korea Kusini kwa saa 2:05:20.

Akizungumza wakati wa kumpokea mwanariadha huyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kamanda wa kikosi namba 833 KJ JKT Oljoro anakofanya kazi nyota huyo, Kanali Victor Faustine amempongeza Neema kwa jitihada za kuitangaza nchi kimataifa kupitia michezo.

Amesema Neema ni mtu ambaye anajituma, mwaminifu na mwadilifu jambo ambalo limemfanya aendelee kung’ara katika mashindano mbalimbali ambayo amekuwa akishiriki.

“Jukumu la Jeshi la Wananchi na Jeshi la kujenga Taifa ni kuibua vipaji na kuendelea kuwalea vijana ili kuweza kuwa na mchango mkubwa katika Taifa,” amesema Faustine.

Mjumbe wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Alfredo Shahanga amesema ushindi wa nyota huyo imezidi kuwatangaza kama wasimamizi wa mchezo huo ukizingatia kwenye riadha wanawake wamekuwa ni wachache.

“Nawapongeza JKT kwa kufanya kazi ya kuwalea wanariadha wengi kwani tulionao wengi wanatoka katika timu za majeshi,” amesema Shahanga.

Kwa upande wake, Neema Msuadi ameweka wazi kuwa mbio hazikuwa rahisi kutokana na ushindani uliokuwepo baina ya wanariadha kutoka mataifa mengine ambao walishiriki.

“Niipongeza JKT kwa kuendelea kutulea katika maadili mazuri pia nashukuru kwa hamasa kubwa kwenye mapokezi yangu”, amesema Neema.