KAMA kuna mashabiki waliinjoi leo kwa Mkapa basi ni kushuhudia shoo ya Mwimbaji wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuph Kirungi maarufu kama Mbosso.
Kama kuna tuzo zingetolewa za ‘man of the show’ msanii huyo alikuwa anaondoka nayo kutokana na namna alivyoingia hadi anamaliza kuburudisha mashabiki waliokuwa wanainjoi burudani kutoka kwa mkali huyo wa wimbo wa Pawa.
Wala hakukuwa na mambo ya kushoto, kulia, mikono juu wala mpige bao asiyeimba kila ngoma aliyoanza kuimba wala hakupata tabu jukwaa liliimba naye.
Mbosso alikuwa msanii wa mwisho kupanda jukwaani awali walipanda wanamuziki kama Chino, Joh Makini na wengineo na aliingia saa 11:02 kisha akamaliza 12:05 takribani saa 1 na dakika tatu.

Mkali huyo wa Pawa aliingia kitofauti, alitinga kwa Mkapa na magari zaidi ya matatu ambayo yalichorwa rangi na kubeba madansa wake ambao nao walijichora rangi kwenye nguo zao.
Mbosso aliingia saa 11:03 jioni saa 12:05
Aliingilia lango la kaskazini mashariki mwa uwanja wa Benjamin Mkapa akiwa yeye na madansa wake bila magari yake.
Wimbo wa kwanza kupafomu ulikuwa Sele akiwatanguliza watu wafupi, kama ilivyokuwa kwenye video ya wimbo huo uliotoka mwaka jana akimshirikisha mwimbaji kutoka Afrika Kusini, Chley wenye zaidi ya watazamaji Milioni nne YouTube.
Alipomaliza kuimba wimbo wa kwanza Sele, akanyamaza kwa dakika moja, akaibua shangwe uwanja mzima.
Shoo ya Mbosso ambaye aliimba kwa muda mrefu ilionekana kupangili vizuri kwani hata madansa wake walijigawa makundi matano, upande wa kaskazini, kusini, jukwaani na mbele ya jukwaa. Pia wapo waliokuwa wamesimama wakiigiza kulinda.

Kama kuna shoo ambayo Mbosso atakuwa ameinjoi kufanya ni hiyo ya Simba Day kutokana na kiu yake ya kuimba mbele ya timu yake pendwa Simba.
Hii ni shoo ya kwanza kwa Mbosso kupafomu Simba Day akiwa msanii pekee aliyeimba kwa muda mrefu na akaitendea haki shoo hiyo.
Kila ngoma aliyoimba ilionekana kukosha mashabiki wa Mnyama waliojaa kiwanjani kushuhudia tamasha hilo la 17.
Achana na ngoma alizoimba kama Kunguru, Aviola na nyinginezo ambazo aliibua vaibu lakini nyimbo mbili za Pawa na Haijakaa Sawa alizoimba live zilimpa thamani kubwa na kupongezwa na mashabiki.
Hilo lilionyesha uwezo wake mwingine wa kuimba live ambalo wasanii wengine kama Joh Makini, Chino na wengine waliimba kwa biti.


MBO 04
ZUBEDA ASIMAMA DAKIKA MOJA
Burudani aliyotoa Mbosso kwenye kilele cha wiki ya Simba Day imeonekana kumkosha, Mtendaji wa Simba Zubeda Sakuru.
Kwenye shoo hiyo ambayo iliibua shangwe kubwa la mashabiki hasa kwenye wimbo wa Sele, Zubeda alionekana kuupenda Nusu Saa akiinuka kwenye kiti alichokaa na kuanza kucheza.
Mtendaji huyo alisimama kwa dakika moja akicheza na kuimba wimbo huo hasa mstari wa verse ya pili ambao Mbosso alitoa kwenye wimbo wa Kitambaa Cheupe wa hayati King Kikii.

Wakati Mbosso anapafomu Aviola, mkurugenzi wa lebo ya King Music, Ali Kiba alikuwa akizunguka uwanja mzima akihamasisha mashabiki kushangilia.
AliKiba hakupafomu, lakini ni kama alikwenda kumpa sapoti Mbosso ambaye alikuwa na shoo nzuri siku hiyo.
Baada ya kuuzunguka uwanja mzima akaenda alipokuwa Mbosso na kucheza kidogo kisha akaondoka na kumuacha Khan aendelee na shoo hiyo.