UTAMBULISHO wa kikosi cha Simba SC kwa msimu wa 2025-2026, umeteka hisia za mashabiki wa timu hiyo waliofika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku mastaa wawili Shomari Kapombe na Elie Mpanzu wakiibua shangwe lililopitiliza.
Zoezi hilo la utambulisho lililoanza saa 12:21 jioni, liliongozwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally na kutamatika saa 12:55 jioni, jumla ya wachezaji 31 wakitambulishwa.
Katika wachezaji hao, wapo watatu waliopandishwa kutoka timu ya vijana ya Simba ambapo Ally amesema wataonekana na kikosi cha wakubwa kwa msimu wa 2025-2026.
Utambulisho huo ulioanza kwa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, lina jumla ya watu 13 ambao wametambulishwa mbele ya mashabiki wa Simba.
Baada ya utambulisho wa benchi la ufundi, Ally aliwaita vijana watatu waliopandishwa timu ya wakubwa.
Wakati wa utambulisho wa wachezaji wengine baada ya hao vijana, Kapombe aliyekuwa wa 12 kutambulishwa, Ally aliwaambia mashabiki wasimame kwa heshima yake kutokana na ukongwe alionao ndani ya Simba.
Kapombe aliyeitumikia Simba kwa vipindi viwili, alianza 2011 alipojiunga nayo akitokea Polisi Morogoro, mwaka 2013 akaondoka na kutua AS Cannes ya Ufaransa, kisha akarudi nchini na kutua Azam kabla ya 2017 kusajiliwa tena na Simba ambapo yupo hadi sasa akiwa na takribani miaka kumi ya utumishi wake ndani ya Msimbazi.
Mwingine aliyeibua shangwe zaidi ni Elie Mpanzu, hiyo ilitokana na Ally kuchagiza kwamba kuna watu walimmezea mate, lakini akaamua kuendelea kuitumikia Simba.
Alassane Kante, Joshua Mutale, Mohamed Bajaber, Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah, nao walikuwa miongoni mwa walioteka hisia za mashabiki wakati wa utambulisho wao.
KIKOSI KILICHOTAMBULISHWA
Moussa Camara, Husein Abel, Yakoub Suleiman, David Kameta ‘Duchu’, Antony Mligo, Naby Camara, Abdulrazack Hamza, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, Vedastus Masinde, Wilson Nangu na Shomari Kapombe.
Wengine ni Yusuph Kagoma, Alassane Kante, Awesu Awesu, Morice Abraham, Kibu Denis, Hussein Daud Semfuko, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Mohamed Bajabir, Ladack Chasambi na Neo Maema.
Pia wapo Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu, Steven Mukwala, Seleman Mwalimu na Jonathan Sowah.